Wagalatia 3

Wagalatia 3

Sheria au imani

1Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulubiwa?

2Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

3Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?

4Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli.

5Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

6Kama vile Abrahamu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.[#Mwa 15:6; Rum 4:3]

7Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Abrahamu.[#Rum 4:16]

8Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiria Abrahamu Habari Njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.[#Mwa 12:3; 18:18; Mdo 3:25]

9Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Abrahamu aliyekuwa mwenye imani.[#Rum 4:16]

10Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Torati, ayafanye.[#Kum 27:26]

11Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.[#Hab 2:4; Rum 1:17; Ebr 10:38]

12Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.[#Law 18:5; Rum 10:5]

13Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;[#Kum 21:23; Rum 8:3; 2 Kor 5:21]

14ili kwamba baraka ya Abrahamu iwafikie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.

Ahadi kwa Abrahamu

15Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno.

16Basi ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazawa, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.[#Mwa 12:7; 13:15; 17:7; 22:18; 24:7]

17Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.[#Kut 12:40]

18Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa njia ya ahadi.[#Rum 4:14; 11:6]

Kusudi ya Torati

19Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hadi aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.[#Rum 5:20; Ebr 2:2; Mdo 7:38,53]

20Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja.

21Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, hakika haki ingalipatikana kwa sheria.[#Rum 8:2-4]

22Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.[#Rum 3:9-19; 11:32]

23Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.[#Gal 4:3; 1 Pet 1:5]

24Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.

25Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.[#Rum 10:4]

26Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.[#Yn 1:12; Rum 8:17]

27Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.[#Rum 6:3; 13:14]

28Hakuna Myahudi wala Mgiriki. Hakuna mtumwa wala huru. Hakuna mwanamume wala mwanamke. Maana ninyi nyote mmekuwa wamoja katika Kristo Yesu.[#Rum 10:12; 1 Kor 12:13]

29Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Abrahamu, na warithi kulingana na ahadi.[#Rum 4:13; 9:7]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya