Hagai 2

Hagai 2

Utukufu wa hekalu ujao

1Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

2Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hao watu waliokuwa wamebaki, ukisema,

3Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?[#Ezr 3:12; Zek 4:10]

4Lakini sasa uwe jasiri, Ee Zerubabeli, asema BWANA; nawe uwe jasiri, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni jasiri, enyi watu wote wa nchi hii, asema BWANA; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema BWANA wa majeshi;[#Zek 8:9; Kut 3:12; 1 Sam 16:18; Hag 1:13; Mk 16:20; Rum 8:31]

5kama ilivyo ahadi niliyowawekea mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope.[#Kut 29:45-46; Neh 9:20; Isa 63:11; Zek 4:6]

6Kwa maana BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa mara nyingine, kitambo kidogo tu, nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;[#Ebr 12:26; Isa 34:4; Yer 4:26]

7nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema BWANA wa majeshi.[#Mwa 3:15; Kum 18:15; Mal 3:1; Zab 24:7]

8Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi.

9Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi.[#Yn 1:14; Lk 11:31; 2:14; Zab 85:8,9; Isa 9:6]

Karipio na ahadi

10Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

11BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani kuhusu sheria, mkisema,[#Law 10:10; Kum 33:10]

12Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye kwa upindo wake akagusa mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula chochote, je, Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La.

13Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je, Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi.[#Hes 19:11-22]

14Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi.[#Tit 1:15]

15Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla jiwe halijatiwa juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA;[#Hag 1:5]

16katika wakati huo wote, mtu alipofikia rundo la vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia pipa kubwa apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu.

17Niliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.[#Kum 28:22; 1 Fal 8:37; Yer 5:3; Amo 4:6-11]

18Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya.[#Zek 8:9]

19Je, Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.

Ahadi ya Mungu kwa Zerubabeli

20Kisha neno la BWANA likamjia Hagai mara ya pili, siku ya ishirini na nne ya mwezi, kusema,

21Sema na Zerubabeli, mtawala wa Yuda, ukisema, Nitazitikisa mbingu na dunia;[#Eze 21:27; Ebr 12:26]

22nami nitakipindua kiti cha enzi cha falme, nami nitaziharibu nguvu za falme za mataifa; nami nitayapindua magari, na hao wapandao ndani yake; farasi na hao wawapandao wataanguka chini; kila mtu kwa upanga wa ndugu yake.[#Dan 2:44; Mt 24:7; Mik 5:10]

23Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitakutwaa wewe, Ee Zerubabeli, mtumishi wangu, mwana wa Shealtieli, asema BWANA, nami nitakufanya kuwa kama pete yenye mhuri; kwa kuwa nimekuchagua, asema BWANA wa majeshi.[#Wim 8:6; Yer 22:24; Isa 42:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya