Waraka kwa Waebrania 1

Waraka kwa Waebrania 1

Mungu amenena katika mwanaye

1Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,

2mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.[#Zab 2:8; Yn 1:3; Kol 1:16; Mt 21:38]

3Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wa Mungu na chapa kamili ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi katika mkono wa kulia wa Ukuu huko juu;[#Zab 110:1; 2 Kor 4:4; Kol 1:15; Mk 16:19; Ebr 9:14,26]

4amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.[#Flp 2:9]

Mwana ni mkuu kuliko Malaika

5Kwa maana ni kwa malaika yeyote yupi Mungu,[#Zab 2:7; 2 Sam 7:14; 1 Nya 17:14; Ebr 5:5; Mdo 13:33]

Ndiwe mwanangu,

Mimi leo nimekuzaa?

Na tena

Mimi nitakuwa kwake baba,

Na yeye atakuwa kwangu mwana?

6Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema,[#Kum 32:43; Rum 8:29; Zab 97:7]

Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.

7Na kuhusu malaika asema,[#Zab 104:4]

Awafanya malaika wake kuwa pepo,

Na watumishi wake kuwa miali ya moto.

8Lakini kuhusu Mwana asema,[#Zab 45:6-7]

Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele;

Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya haki.

9Umependa haki, umechukia maasi;

Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta,

Mafuta ya shangwe kupita wenzio.

10Na tena,[#Zab 102:25-27]

Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi,

Na mbingu ni kazi za mikono yako;

11Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu;

Nazo zote zitachakaa kama nguo,

12Na kama mavazi utazikunjakunja, na kama mavazi zitabadilishwa;

Lakini wewe u yeye yule,

Na miaka yako haitakoma.

13Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wowote,[#Zab 110:1]

Uketi mkono wa kulia

Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako?

14Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?[#Dan 7:10; Zab 34:8; 91:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya