Isaya 47

Isaya 47

Kuaibishwa kwa Babeli

1Haya, shuka, keti mavumbini,[#Yer 48:18; Omb 2:3,10; Isa 13:1—14:23; Yer 50:1—51:64]

Ewe bikira, binti Babeli;

Keti chini pasipo kiti cha enzi,

Ewe binti wa Wakaldayo;

Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa.

2Twaa mawe ya kusagia, usage unga;[#Kut 11:5]

Vua utaji wako, ondoa mavazi yako,

Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.

3Uchi wako utafunuliwa,[#Nah 3:5; Mt 7:2; Rum 12:19]

Naam, aibu yako itaonekana.

Nitalipa kisasi; simkubali mtu yeyote.

4Mkombozi wetu, BWANA wa majeshi ndilo jina lake,

Mtakatifu wa Israeli.

5Kaa kimya, ingia gizani,[#1 Sam 2:9; Dan 2:37]

Ee binti wa Wakaldayo;

Maana hutaitwa tena Malkia wa falme.

6Nilikuwa nimekasirika na watu wangu, niliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; kwa wazee uliifanya nira yako kuwa nzito sana.[#2 Nya 28:9; Isa 10:6; Zek 1:15; Kum 28:50]

7Ukasema, Mimi nitakuwa malkia milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo.[#Ufu 18:7]

8Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi kama mjane, wala sitajua kufiwa na watoto;[#Sef 2:15; Ufu 18:7-8]

9lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kamili, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.[#1 The 5:3; Dan 2:2; Nah 3:4; 2 The 2:9,10; Ufu 9:21]

10Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi.[#Zab 52:7; Eze 8:12]

11Kwa sababu hiyo uovu utakupata; wala hutaweza kuuagua; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa usioujua utakupata kwa ghafla.[#Isa 13:6; Dan 5:30; Lk 17:27]

12Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda.

13Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wanajimu, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe kutoka kwa mambo yatakayokupata.

14Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa kutoka kwa nguvu za muali wa moto; hili halitakuwa kaa la kujipasha moto, wala moto wa kuota.[#Nah 1:10; Mal 4:1]

15Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatangatanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.[#Ufu 18:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya