Yeremia 13

Yeremia 13

Kitani cha kiunoni

1BWANA akaniambia hivi, Nenda ukajinunulie kitambaa cha kitani, ukajifunge kiunoni, wala usikitie majini.

2Basi nikanunua kitambaa cha kitani sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni.

3Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema,

4Twaa kitambaa kile ulichonunua, kilicho viunoni mwako, kisha ondoka, nenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali.[#Zab 137:1; Mik 4:10]

5Basi nikaenda, nikakificha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru.

6Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, nenda mpaka mto Frati, ukakitwae kile kitambaa, nilichokuamuru kukificha huko.

7Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikakitwaa kile kitambaa katika mahali pale nilipokificha; na tazama, kitambaa kilikuwa kimeharibika, hakikufaa tena kwa lolote.[#Isa 64:6; Yer 24:8; Omb 3:45]

8Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema,

9BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu.[#Law 26:19]

10Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na kitambaa hiki kisichofaa kwa lolote.[#2 Nya 36:15,16; Yer 9:14; 11:8]

11Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.[#Mwa 17:7; Kut 19:5; Yer 33:9]

Ishara ya chupa ya mvinyo

12Basi utawaambia neno hili, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai?

13Ndipo utakapowaambia, BWANA asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu.[#Zab 60:3; Isa 63:6; Yer 25:27; Eze 23:32-34; Ufu 14:10]

14Nitawagonganisha, mtu na mwenzake, naam, baba za watu na watoto wao pamoja, asema BWANA; sitahurumia, wala sitaachilia, wala sitarehemu, hata nisiwaangamize.

Tishio la kupelekwa uhamishoni

15Sikilizeni ninyi, kategeni masikio yenu; msifanye kiburi; maana BWANA amenena.[#Kum 32:29]

16Mtukuzeni BWANA, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, na kabla miguu yenu haijakwaa juu ya milima yenye giza; na wakati mnapoitazamia nuru, kabla hajaigeuza kuwa kivuli cha mauti, na giza nene.[#Yos 7:19; 1 Sam 6:5; Yoe 2:12; Amo 8:9; Isa 5:30; 59:9; Zab 44:19]

17Bali kama hamtaki kusikia, roho yangu italia kwa siri, kwa sababu ya kiburi chenu; na jicho langu litalia sana na kutoka machozi mengi, kwa kuwa kundi la BWANA limechukuliwa mateka.

18Mwambie mfalme, na mama ya mfalme,[#2 Fal 24:12]

Nyenyekeeni na kuketi chini;

Kwa maana vilemba vyenu vimeshuka,

naam, taji la utukufu wenu.

19Miji ya Negebu imefungwa malango yake,[#Law 26:31]

wala hapana mtu wa kuyafungua;

Yuda amechukuliwa mateka;

amechukuliwa kabisa mateka.

20Inua macho yako, Ee Yerusalemu, ukawatazame hawa wanaokuja kutoka kaskazini; liko wapi kundi lako ulilopewa, kundi lile zuri?[#Yer 6:22]

21Utasema nini wewe, atakapowaweka rafiki zako kuwa kichwa juu yako, ikiwa wewe mwenyewe umewafundisha kuwa juu yako? Je! Huzuni haitakushika, kama uchungu wa mwanamke aliye katika kuzaa?

22Nawe ukisema moyoni mwako, Mbona mambo haya yamenipata mimi? Ni kwa sababu ya wingi wa uovu wako, marinda yako yamefunuliwa, na visigino vya miguu yako vimeumia.[#Yer 16:10; Isa 47:2; Nah 3:5]

23Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoadoa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.

24Kwa sababu hiyo nitawatawanya, kama makapi yapitayo, kwa upepo wa jangwani.

25Hiyo ndiyo kura yako, fungu lako ulilopimiwa na mimi, asema BWANA; kwa kuwa umenisahau, na kuutumainia uongo.[#Ayu 20:29; Yer 10:14; Mik 3:11]

26Kwa ajili ya hayo, mimi nami nitayafunua marinda yako mbele ya uso wako, na aibu yako itaonekana.[#Omb 1:8; Hos 2:10]

27Nimeona machukizo yako, naam, uzinifu wako, na ubembe wako, na uasherati wa ukahaba wako, juu ya milima katika mashamba. Ole wako, Ee Yerusalemu! Hutaki kutakaswa; mambo hayo yataendelea hata lini?[#Yer 5:8; 2:20; Isa 65:7]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya