Ayubu 10

Ayubu 10

Nayachukia maisha yangu

1Nayachukia maisha yangu;

Nitayasema malalamiko yangu wazi;

Nitanena kwa uchungu wa roho yangu.

2Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa;

Nijulishe kwa nini unapingana nami.

3Je! Ni vema kwako wewe kuonea,

Na kuidharau kazi ya mikono yako,

Na kuiunga mkono mipango ya waovu?

4Je! Wewe una macho ya kimwili,[#1 Sam 16:7; Lk 16:15; Ufu 1:14]

Au je! Waona kama aonavyo binadamu?

5Je! Siku zako ni kama siku za mtu,

Au je! Miaka yako ni kama miaka ya mtu,

6Hata ukaulizauliza habari za uovu wangu,

Na kuitafuta dhambi yangu,

7Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu;

Wala hapana awezaye kuokoa kutoka kwa mkono wako?

8Mikono yako imeniumba na kunifinyanga;[#Zab 119:73; Isa 43:7]

Nawe utageuka na kuniangamiza?

9Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo;[#Mwa 2:7; Isa 45:9]

Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena?

10Je! Wewe hukunimimina kama maziwa,[#Zab 139:14]

Na kunigandisha mfano wa jibini?

11Umenivika ngozi na nyama,

Na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa.

12Unanijalia uhai na fadhili,

Na kwa uangalifu wako roho yangu imetunzwa.

13Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako;

Najua kuwa haya yamo nafsini mwako;

14Nikifanya dhambi, ndipo waniangalia,

Wala hutaniachilia na uovu wangu.

15Mimi nikiwa mwovu, ole wangu![#Zab 9:17; Isa 3:11; Mal 3:18; Ayu 9:12; Kut 3:7; Zab 25:18; Omb 1:20]

Nami nikiwa mwenye haki, walakini sitainua kichwa changu;

Maana nimejaa aibu

Nikiyaangalia mateso yangu.

16Kichwa changu kikijiinua, waniwinda kama simba;[#Isa 38:13; Omb 3:10]

Tena wajionesha kwangu kuwa wa ajabu.

17Wewe unafanya upya ushahidi wako juu yangu,

Na kuongeza kisirani chako juu yangu;

Ukileta jeshi baada ya jeshi juu yangu.

18Kwa nini basi kunitoa tumboni?

Ningekata roho, lisinione jicho lolote.

19Ningalikuwa kama mtu asiyekuwapo;

Ningalichukuliwa kaburini kutoka tumboni.

20Je! Siku zangu si chache? Acha basi,[#Zab 39:13; Ayu 7:16]

Usinisumbue, nipate angaa kutulizwa moyo kidogo.

21Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena,[#Ayu 3:5; Zab 88:12; 23:4]

Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu;

22Ni nchi ya giza kuu, kama giza lenyewe lilivyo;

Ni nchi ya giza tupu, isiyo na mpango wowote wa mambo,

Nchi ambayo nuru yake ni kama giza.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya