Mambo ya Walawi 24

Mambo ya Walawi 24

Taa isiyozimika

1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2Waagize wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima.[#Kut 27:20; 39:37; Hes 8:2-4]

3Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeneza tangu jioni hadi asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.

4Atazitengeneza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za BWANA daima.[#Kut 31:8; 37:17-24]

Mikate ya Hema Takatifu

5Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja.[#Kut 25:30; 40:24]

6Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za BWANA.[#1 Fal 7:48; 2 Nya 4:19; Ebr 9:2]

7Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto.

8Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za BWANA daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele.[#Hes 4:7; 1 Nya 9:32; 2 Nya 2:4]

9Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zitolewazo kwa BWANA kwa moto, kwa amri ya milele.[#Mt 12:4; Mk 2:26; Lk 6:4; 1 Sam 21:6; Kut 29:33; Law 8:3; 21:22]

Kufuru na adhabu yake

10Ikawa mwanamume mmoja ambaye mama yake ni Mwisraeli, na babaye ni Mmisri, alitokea kati ya wana wa Israeli akalikufuru; na kupigana na Mwisraeli katika kambi;

11kisha huyo mwanamume ambaye mama ni Mwisraeli akakufuru jina la Bwana na kulaani nao watu wakampeleka kwa Musa. Mama yake mtu huyo alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila la Dani.[#Ayu 1:5; 2:5,9; Isa 8:21; Kut 18:22]

12Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa BWANA.[#Hes 15:34; Kut 18:15,16]

13Na BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

14Mtoe huyo aliyelaani nje ya kambi; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe.[#Kum 17:7]

15Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu yeyote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake.[#Law 5:1; 9:13]

16Na yeyote atakayelaani jina la BWANA hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzaliwa, hapo atakapolaani jina la BWANA atauawa.[#1 Fal 21:10; Zab 74:10,18; Mt 12:31; Mk 3:28; Yak 2:7]

17Na mtu ampigaye mtu hadi akafa, lazima atauawa;[#Kut 21:12; Mwa 9:6; Hes 35:31; Kum 19:11; Mt 26:52; Ufu 13:10]

18na atakayempiga mnyama hadi akafa atalipa; uhai kwa uhai.

19Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo hivyo;[#Kut 21:24; Kum 19:21; Mt 5:38; 7:2]

20jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo hivyo.[#Kut 21:23-25; Kum 19:21; Mt 5:38]

21Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa.[#Kut 21:33]

22Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Hes 15:16; Kut 12:49; Law 19:34; Kum 10:17,19]

23Musa akanena na wana wa Israeli, nao wakamtoa huyo aliyeapiza nje ya kambi, wakamwua kwa kumpiga kwa mawe. Wana wa Israeli wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa.[#Kum 13:9; 17:7]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya