The chat will start when you send the first message.
1Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari.[#Mk 4:1-20; Lk 8:4-15]
2Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda katika mashua, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.[#Lk 5:1-3]
3Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.
4Na alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
5nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; zikaota haraka, kwa kukosa udongo wenye kina;
6Lakini jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.
7Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
8nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
9Mwenye masikio na asikie.
10Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?
11Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.
12Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.[#Mt 25:29; Mk 4:25; Lk 8:18; 19:26]
13Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa.[#Kum 29:4]
14Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema,[#Isa 6:9-10; Yn 12:40; Mdo 28:26,27]
Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa;
Kutazama mtatazama, wala hamtaona.
15Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito,
Na kwa masikio yao hawasikii vema,
Na macho yao wameyafumba;
Wasije wakaona kwa macho yao,
Wakasikia kwa masikio yao,
Wakaelewa kwa mioyo yao,
Wakaongoka, nikawaponya.
16Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.[#Lk 10:23-24]
17Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
18Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi.
19Kila mtu alisikiapo neno la ufalme bila kulielewa, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.
20Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha;
21lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.
22Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai.[#Mt 6:19-34; 1 Tim 6:9]
23Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kulielewa; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.
24Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake;[#Mt 13:36-43]
25lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.
26Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.
27Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Limepata wapi basi magugu?
28Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?
29Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo.
30Viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.[#Mt 3:12]
31Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake;[#Mk 4:30-32; Lk 13:18,19]
32nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko miboga yote ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake.[#Dan 4:12,21; Eze 17:23; 31:6; Zab 104:12]
33Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.[#Lk 13:20,21]
34Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno;[#Mk 4:33,34]
35ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,[#Zab 78:2]
Nitafumbua kinywa changu kwa mifano,
Nitayatamka yaliyositirika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
36Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia katika nyumba; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya shambani.[#Mt 13:24-30]
37Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;
38lile shamba ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;[#1 Kor 3:9]
39yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.
40Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.[#Yn 15:6]
41Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,[#Sef 1:3; Mt 25:31-46; 7:23]
42na kuwatupa katika tanuri ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.[#Mt 8:12]
43Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.[#Dan 12:3]
44Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.[#Mt 19:29; Lk 14:33; Flp 3:7; Mit 2:4]
45Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
46naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.[#Mit 8:10,11]
47Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;[#Mt 22:9,10]
48hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa.
49Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki,[#Mt 25:32]
50na kuwatupa katika tanuri ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
51Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.
52Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.
53Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.[#Mk 6:1-6; Lk 4:15-30]
54Na alipofika mji wa kwao, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?[#Mt 7:28; 11:1; 19:1; 26:1]
55Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?
56Na dada zake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?[#Yn 7:15,52]
57Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe.[#Yn 4:44]
58Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutoamini kwao.