Zaburi 114

Zaburi 114

Maajabu ya Mungu wakati wa kutoka Misri

1Haleluya.[#Kut 12:51]

Israeli alipotoka Misri,

Na Yakobo katika watu wa lugha ya kigeni.

2Yuda ilikuwa patakatifu pake,

Israeli milki yake.

3Bahari iliona ikakimbia,[#Kut 14:21; Yos 3:16]

Yordani ilirudishwa nyuma.

4Milima iliruka kama kondoo dume,[#Zab 29:6; 68:16; Hab 3:6]

Vilima kama wana-kondoo.

5Ee bahari, una nini, ndio ukimbie?

Yordani, ndio urudi nyuma?

6Enyi milima, ndio mruke kama kondoo dume?

Enyi vilima, kama wana-kondoo?

7Tetemeka, Ee nchi, mbele za uso wa Bwana,

Mbele za uso wa Mungu wa Yakobo.

8Augeuzaye mwamba kuwa ziwa la maji,[#Kut 17:1-7; Hes 20:2-13; Zab 107:35]

Jiwe gumu kuwa chemchemi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya