Zaburi 19

Zaburi 19

Utukufu wa Mungu katika viumbe na hukumu

1Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,[#Isa 40:22; Rum 1:19]

Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.

2Mchana husemezana na mchana,

Usiku hutolea usiku maarifa.

3Hakuna usemi wala maneno,

Sauti yao haisikilikani.

4Sauti yao imeenea duniani kote,[#Rum 10:18]

Na maneno yao hadi miisho ya ulimwengu.

Katika hizo ameliwekea jua hema,

5Nalo hutokeza kama bwana arusi akitoka chumbani mwake,[#Mhu 11:7]

Lafurahi kama mtu aliye hodari

Kwenda mbio katika njia yake.

6Kuchomoza kwake ni katika mwisho wa mbingu,[#Mhu 1:5]

Na kuzunguka kwake ni hadi miisho ya mbingu,

Wala hakuna kitu

Kisichofikiwa na joto lake.

7Sheria ya BWANA ni kamilifu,

Huiburudisha nafsi.

Ushuhuda wa BWANA ni amini,

Humtia hekima mtu asiye nayo.

8Maagizo ya BWANA ni ya adili,[#Neh 9:13; Rum 7:12]

Huufurahisha moyo.

Amri ya BWANA ni safi,

Huyatia macho nuru.

9Kicho cha BWANA ni kitakatifu,

Kinadumu milele.

Hukumu za BWANA ni kweli,

Zina haki kabisa.

10Ni za kutamanika kuliko dhahabu,

Kuliko wingi wa dhahabu safi.

Nazo ni tamu kuliko asali,

Kuliko sega la asali.

11Tena mtumishi wako huonywa kwazo,[#Mit 6:22,23]

Katika kuzishika kuna thawabu kuu.

12Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake?

Unitakase na mambo ya siri.

13Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi,

Yasinitawale mimi.

Ndipo nitakapokuwa kamili,

Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.

14Maneno ya kinywa changu,[#Isa 44:6]

Na mawazo ya moyo wangu,

Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA,

Mwamba wangu, na mwokozi wangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya