The chat will start when you send the first message.
1Ee BWANA, nakuinulia nafsi yangu,[#1 Sam 1:15; Zab 86:4; Omb 3:41]
2Ee Mungu wangu,[#Zab 7:1; 18:2; Rum 10:11]
Nimekutumainia Wewe, nisiaibike,
Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.
3Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja;
Wataaibika watendao uhaini bila sababu.
4Ee BWANA, unijulishe njia zako,[#Kut 33:13; Zab 143:8; Mit 8:20]
Unifundishe mapito yako,
5Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana kutwa.
6Ee BWANA, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
7Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,[#Zab 51:1]
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee BWANA kwa ajili ya wema wako.
8BWANA yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
9Wenye upole atawaongoza katika haki,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
10Njia zote za BWANA ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
11Ee BWANA, kwa ajili ya jina lako,[#Zab 31:3; 79:9; Rum 5:20]
Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi.
12Ni nani amchaye BWANA?[#Zab 37:23]
Atamfundisha katika njia anayoichagua.
13Watafanikiwa maishani mwao;[#Zab 37:11,22,29]
Na wazawa wao wataimiliki nchi.
14Siri ya BWANA iko kwao wamchao,[#Mit 3:32; Yn 7:17; 2 Kor 4:2-6]
Naye atawajulisha agano lake.
15Macho yangu humwelekea BWANA daima,[#Zab 141:8]
Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.
16Uniangalie na kunifadhili,[#Zab 69:16]
Maana mimi ni mkiwa na mteswa.
17Uniondolee shida za moyo wangu,
Na kunitoa katika dhiki zangu.
18Utazame mateso yangu na taabu yangu;[#2 Sam 16:12]
Unisamehe dhambi zangu zote.
19Uwatazame adui zangu, maana ni wengi,
Na kwa namna wanavyonichukia kwa ukatili mwingi.
20Unilinde nafsi yangu na kuniokoa,
Usiniache niaibike, maana nakukimbilia Wewe.
21Ukamilifu na unyofu zinihifadhi,
Maana nakungoja Wewe.
22Ee Mungu, umkomboe Israeli,[#Zab 130:8]
Katika taabu zake zote.