Zaburi 29

Zaburi 29

Sauti ya Mungu katika dhoruba

1Mpeni BWANA, enyi wana wa Mungu,[#Zab 96:7-9; 1 Nya 16:28,29]

Mpeni BWANA utukufu na nguvu;

2Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;

Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.

3Sauti ya BWANA inasikika juu ya maji;

Mungu wa utukufu apiga radi;

BWANA yu juu ya maji mengi.

4Sauti ya BWANA ina nguvu;

Sauti ya BWANA ina utukufu;

5Sauti ya BWANA yaivunja mierezi;

Naam, BWANA aivunjavunja mierezi ya Lebanoni;

6Airusharusha Lebanoni kama ndama wa ng'ombe;[#Zab 114:4; Kum 3:9]

Lebanoni na Sirioni kama mwananyati.

7Sauti ya BWANA inatoa miale paa ya moto;

8Sauti ya BWANA yalitetemesha jangwa;[#Hes 13:26]

BWANA alitetemesha jangwa la Kadeshi.

9Sauti ya BWANA yawazalisha ayala,

Na kuiacha misitu wazi;

Na ndani ya hekalu lake

Wanasema, Utukufu!

10BWANA aketi juu ya Gharika;[#Zab 93:4]

Naam, BWANA ameshika hatamu ya ufalme milele.

11BWANA na awape watu wake nguvu;[#Isa 40:29]

BWANA na awabariki watu wake kwa amani.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya