Zaburi 30

Zaburi 30

Shukrani kwa kuponywa maradhi mabaya

1Ee BWANA, nitakutukuza kwa maana umeniinua,

Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.

2Ee BWANA, Mungu wangu,[#Zab 6:2-4]

Nilikulilia ukaniponya.

3Umeniinua nafsi yangu,[#Zab 40:1,2]

Ee BWANA, kutoka kuzimu.

Umenihuisha na kunitoa

Miongoni mwao washukao Shimoni.

4Mwimbieni BWANA zaburi,

Enyi watauwa wake.

Na kutoa shukrani.

Kwa kukumbuka utakatifu wake.

5Maana ghadhabu zake ni za muda mfupi tu;[#Zab 16:11; Ufu 22:17]

Radhi yake ni ya milele.

Kilio huweza kuwapo usiku,

Lakini furaha huja asubuhi.

6Nami nilipofanikiwa nilisema,[#Ayu 29:18]

Sitaondoshwa milele.

7BWANA, kwa radhi yako[#Zab 104:29]

Wewe uliuimarisha mlima wangu.

Uliuficha uso wako,

Nami nikafadhaika.

8Ee BWANA, nilikulilia Wewe,

Naam, kwa BWANA niliomba dua.

9Mna faida gani katika damu yangu[#Zab 115:17]

Nishukapo Shimoni?

Mavumbi yatakusifu?

Yatautangaza uaminifu wako?

10Ee BWANA, usikie, unirehemu,[#Zab 4:1]

BWANA, uwe msaidizi wangu.

11Umegeuza msiba wangu kuwa ngoma;[#2 Sam 6:14]

Umeniondolea huzuni yangu, kunijalia furaha tele.

12Ili nafsi yangu ikusifu,

Wala isinyamaze.

Ee BWANA, Mungu wangu,

Nitakushukuru milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya