Zaburi 5

Zaburi 5

Mwamini Mungu kwa ukombozi kutoka kwa adui

1Ee BWANA, uyasikilize maneno yangu,

Ukuangalie kutafakari kwangu.

2Uisikie sauti ya kilio changu,

Ee Mfalme wangu na Mungu wangu,

Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.

3BWANA, asubuhi utaisikia sauti yangu,[#Zab 30:5]

Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.

4Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya;[#Mal 2:17]

Mtu mwovu hatakaa kwako;

5Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako;[#Zab 14:1; Hab 1:13]

Unawachukia wote watendao uovu.

6Utawaharibu wasemao uongo;

BWANA humchukia mwuaji na mwenye hila

7Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako,[#1 Fal 8:29]

Nitaingia nyumbani mwako;

Na kusujudu kwa kicho,

Nikilielekea hekalu lako takatifu.

8BWANA, uniongoze kwa haki yako,

Kwa sababu yao wanaoniotea.

Uinyoshe njia yako mbele ya uso wangu,

9Maana vinywani mwao hamna uaminifu;[#Rum 3:13]

Moyo wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi,

Ulimi wao hujipendekeza.

10Wewe, Mungu, uwapatilize,

Na waanguke kwa mashauri yao.

Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao,

Kwa maana wamekuasi Wewe.

11Nao wote wanaokukimbilia watafurahi;[#1 Kor 2:9]

Watapiga kelele za furaha daima.

Kwa kuwa Wewe unawahifadhi,

Walipendao jina lako watakufurahia.

12Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki;

BWANA, utamzungushia radhi kama ngao.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya