The chat will start when you send the first message.
1Hekima yote yatoka kwa BWANA,[#Mit 2:6]
Nayo yakaa kwake hata milele.
2Nani awezaye kuhesabu
Mchanga wa bahari na matone ya mvua
Na siku za milele?
3Nani awezaye kutafuta
Kimo cha mbingu na upana wa dunia
Na kina cha bahari?
4Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote,
5Na ufahamu wa busara tangu milele.
6Nani aliyefunuliwa shina la hekima?
7Nani aliyejua mashauri yake merevu?
8Yuko Mmoja aliye na hekima,
Naye yu wa kuogopwa sana,
Ameketi katika kiti chake cha enzi.
9BWANA ndiye aliyeiumba[#Mit 8:22-31; Sira 29:9]
Na kuiona na kuihesabu,
Na kuimwaga juu ya kazi zake zote.
10Ina wote wenye mwili kama aitoavyo,
Na wale wampendao amewapa kwa wingi.
11Kumcha BWANA
Ni heshima na utukufu,
Na furaha na taji la shangwe.
12Kumcha BWANA
Kunachangamsha moyo,
Na kuleta sherehe na maisha kunjufu.
13Kumcha BWANA
Kwamletea mtu heri mwishowe,
Na siku ya kufa kwake atabarikiwa.
14Kumcha BWANA
Ni chanzo cha hekima,
Imeumbwa tumboni pamoja na waamini.
15Kwa watu imekaa tangu awali,
Pia itadumu kwa wazao wao.
16Kumcha BWANA
Ni utimilifu wa hekima,
Inashibisha wanadamu matunda yake.
17Itajaza nyumba pia vitakiwavyo,[#Hek 7:11]
Na ghala zitajazwa mavuno yake.
18Kumcha BWANA
Ni taji la hekima,
Inasitawisha amani na afya nzuri.
19Kumcha BWANA
Ni gongo na nguzo tukufu,
Ni heshima ya daima kwao waishikao.
20Kumcha BWANA[#Mit 3:16; 4:10]
Ni shina la hekima,
21Na matawi yake ni maisha mengi.
22Hasira isiyo haki haiwezi kuthibitishwa,
Maana ukali wa ghadhabu ni maangamizi yake.
23Mtu aliye mvumilivu atastahimili hata wakati ufaao, na hatimaye ukunjufu wa moyo utaanza kukua ndani yake.
24Aidha, ujapo wakati ufaao atayaficha maneno yake, na wengi kwa midomo yao watautangaza ufahamu wake.
25Mithali za elimu zimo kanzini mwa hekima,
Bali utawa ni chukizo kwa mkosefu.
26Ukitamani hekima uzishike amri, naye BWANA atakupa tele;
27yaani, kumcha BWANA ndiyo hekima na mafundisho, tena imani na unyenyekevu ndiyo mapenzi yake.
28Usikatae kumcha BWANA kama una haja,
Wala usimkaribie nawe una nia mbili.
29Usiwe mnafiki machoni pa watu, tena kuhusu midomo yako ufanye hadhari.
30Wewe usijikuze mwenyewe, usije ukaanguka na kujiaibisha roho yako; madhali BWANA atazifunua siri zako, na kukuangamiza katikati ya kusanyiko, kwa sababu hukumfikilia BWANA mwenye kicho, lakini moyo wako umejaa hila.