The chat will start when you send the first message.
1BASSI na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, tuweke kando killa mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa uvumilivu katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
2tukimtazama Yesu, aliveianzisha imani yetu na kuitimiliza; ambae kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele zake aliuvumilia msalaba na kuidharau aibu, nae ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
3Maana mtafakarini sana yeye aliyeyavumilia mapingamizi makuu namna hii ya wenye dhambi juu ya nafsi zao, msije mkadhoofika mkizimia mioyoni mwenu.
4Hamjafanya vita kiasi cha kumwaga damu, mkishindana na dhambi:
5tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama na wana.
Mwanangu, usikudharau kurudi kwake Bwana,
Wala, usizimie ukikemewa nae;
6Maana yeye ambae Bwana humpenda, humrudi,
Nae humpiga killa mwana amkubaliye.
7Ni kwa ajili ya kurudiwa mwavumilia; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiorudiwa na baba yake.
8Bassi kama mkiwa hamna kurudiwa walikoshiriki wote, mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.
9Na pamoja na haya tulikuwa na baba za mwili wetu walioturudi, tukawastahi; bassi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi.
10Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu illi tuushiriki utakatifu wake.
11Killa adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini huwatolea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.
12Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza,
13mkaifanyia miguu yenu njia za kunyoka, illi kitu kilicho kilema kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.
14Fanyeni bidii kutafuta amani kwa watu wote, na utakatifu, ambao hapana mtu atakaemwona Mungu asipokuwa nao;
15mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua watu wengi, wakatiwe najis kwa hilo.
16Asiwepo asharati au asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja.
17Maana mwajua ya kuwa hatta alipotaka baadae kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.
18Maana hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingi jeusi, na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno;
19ambayo wale waliosikia walisihi wasiambiwe neno lo lote lingine; maana hawakuweza kustahimili neno lile lililoamriwa,
20Hatta nyama akiugusa mlima atapigwa mawe au atachomwa kwa mkuki.
21Na baya yaliyoonekana yalikuwa ya kutisha, hatta Musa akasema, Nashikwa na khofu na kutetemeka.
22Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye tiayi, Yerusalemi wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi,
23na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika,
24na Yesu mwenye kuleta agano jipya, na damu ya kunyunyizwa inenayo mema kuliko ile ya Habil.
25Angalieni msimkatae yeye anenae. Maana ikiwa wale hawakuokoka waliomkataa yeye aliyewaonya juu ya inchi, sembuse sisi tukijiepusha nae atuonyae kutoka mbinguni:
26Ambae sauti yake iliitemetesha inchi wakati ule: lakini sasa ameahidi akinena, Marra moja tena naitetemesha inchi wala si inchi tu, bali na mbingu pia.
27Neno lile, Marra moja tena, ladhihirisha kuhamishwa vile viwezavyo kutetemeshwa, kama vitu vilivyoumbwa, illi vitu visivyoweza kutetemeshwa vikae.
28Bassi tukipokea ufalme usioweza kutetemeshwa, tuwe na neema, illi kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho:
29maana Mungu wetu ni moto ulao.