The chat will start when you send the first message.
1Kaka na dada zangu sasa nina mambo mengine ya kuwaambia. Tuliwafundisha namna ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Nanyi mnaishi hivyo. Na sasa tunawaomba na kuwatia moyo katika Bwana Yesu kuishi zaidi na zaidi katika njia hiyo.
2Mnafahamu yote tuliyowaamuru kufanya kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo.
3Mungu anawataka muwe watakatifu. Anawataka mkae mbali na dhambi za zinaa.
4Mungu anawataka kila mmoja wenu ajifunze kuuthibiti mwili wake mwenyewe. Tumieni miili yenu kwa namna iliyo takatifu na yenye heshima.[#4:4 Au “Mungu anamtaka kila mmoja wenu ajue namna ya kutafuta na kupata na kuoa mke kwa namna iliyo takatifu na inayo leta heshima.”]
5Msiruhusu tamaa za mwili kuwatawala kama watu wasiomjua Mungu.
6Msimtendee vibaya ndugu aliye mwamini wala kuwadanganya katika hili. Bwana atawahukumu watendao hivyo. Tumekwisha kuwaambia juu ya hili na kuwaonya.
7Mungu alituita kuwa watakatifu na safi.
8Hivyo kila anayekataa kuyatii mafundisho haya anakataa kumtii Mungu, siyo wanadamu. Na Mungu ndiye anayewapa ninyi Roho Mtakatifu.
9Hatuna haja ya kuwaandikia juu ya kuwa na upendo kwa katika Kristo. Mungu amekwisha kuwafundisha kupendana ninyi kwa ninyi.
10Ukweli ni kuwa, mnawapenda wanaoamini wote walioko Makedonia. Tunawatia moyo sasa, kuuonyesha upendo wenu zaidi na zaidi.
11Fanyeni kila mnaloweza kuishi maisha ya amani. Mjishugulishe na mambo yenu wenyewe, na mfanye kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaambia mwanzo.[#4:11 Au mjipatie fedha zenu wenyewe. Wathesalonike wengi walikuwa watu wenye kufanya kazi za mikono ama vibarua kama vile Paulo mwenyewe alivyokuwa.]
12Mkifanya mambo haya, ndipo wale wasioamini wataheshimu namna mnavyoishi. Na hamtawategemea wengine.
13Kaka na dada, tunawataka mfahamu habari za wale waliokufa. Hatupendi muwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini.
14Tunaamini kuwa Yesu alikufa, ila tunaamini pia kuwa alifufuka. Hivyo tunaamini kuwa Mungu atawaleta katika uzima kupitia Yesu kila aliyekufa na kukusanywa pamoja naye.
15Tunalowaambia sasa ni ujumbe wake Bwana. Sisi ambao bado tu hai Bwana ajapo tena tutaungana nae, lakini hatutawatangulia wale waliokwisha kufa.
16Bwana mwenyewe atakuja kutoka mbinguni pamoja na sauti kuu yenye agizo, na sauti kubwa kutoka kwa malaika mkuu, na ishara ya Mungu ya mlio wa tarumbeta. Na watu waliokufa walio wake Kristo watafufuliwa kwanza.
17Baada ya hayo, sisi ambao bado tungali hai mpaka wakati huo tutakusanywa pamoja na wale waliokwisha kufa. Tutachukuliwa juu mawinguni na kukutana na Bwana angani. Na tutakuwa na Bwana milele.
18Hivyo tianeni moyo ninyi kwa ninyi kwa maneno haya.