The chat will start when you send the first message.
1Nakuamuru mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, ambaye punde atawahukumu wale walio hai na wale waliokwisha kufa na juu ya kuja kwa mara ya pili kwa Kristo kwa sababu kwa hakika atatokea kuja kutawala kama Mfalme:
2Hubiri Ujumbe, uwe tayari kutimiza wajibu wako wakati ulio sahihi hata ule usio sahihi. Wathibitishie watu kwa wanafanya makosa na uwaonye juu ya yale yatakayowatokea. Ufanye hivi kwa subira kubwa na tahadhari katika yale unayofundisha.
3Nasema hivi kwa sababu utakuja wakati ambapo watu hawatakuwa tayari kuyasikiliza mafundisho yenye uzima. Badala yake watawatafuta walimu wanaowapendeza. Watawatafuta walimu wanaosema yale wanayotaka kusikia.
4Na watayageuzia mbali masikio yao kutoka kwenye kweli na kugeukia simulizi za uongo.
5Lakini wewe ujizuie mwenyewe katika mambo yote; vumilia mateso; fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema; ifanye huduma uliyopewa na Mungu.
6Kwangu mimi, nimemiminwa kama kinywaji cha sadaka, na wakati wa kuondoka kwangu kutoka katika maisha haya umekwisha kufika.
7Nimejihusisha katika mashindano ya thamani; nimemaliza mbio; nimeilinda imani.
8Sasa tuzo ya mshindi inaningoja, hii ni taji inatolewa kwa wenye haki. Bwana, aliye hakimu wa haki atanipa taji hiyo katika Siku ile. Ndio atanipa mimi na yeyote mwingine anayengojea kwa dhati kuja kwake.
9Jitahidi kuja kuniona mapema uwezavyo,
10kwani Dema aliniacha kwa sababu aliupenda ulimwengu wa sasa na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia.
11Luka ni peke yake aliyebaki nami. Mchukue Marko na uje naye utakapokuja, kwa sababu anaweza kunisaidia katika kazi yangu.
12Namtuma Tikiko kule Efeso.
13Utakapokuja njoo na koti nililoliacha katika nyumba ya Karpo kule Troa. Pia uniletee vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.
14Iskanda aliye mfua vyuma amenitendea mabaya mengi. Bwana atamlipa kwa yale aliyotenda.
15Wewe pia uwe mwangalifu kwake, kwa kuwa ameyapinga kwa juhudi mafundisho yetu.
16Mara ya kwanza nilipokuwa nafanya utetezi wangu, hakuna hata mmoja aliyekuja kunisaidia. Badala yake wote wakaniacha. Na wasihesabiwe hayo na Mungu.
17Lakini Bwana akasimama upande wangu na kunitia nguvu, ili ujumbe uweze kunenwa nami kwa ukamilifu ili kwamba Mataifa wote waweze kusikia. Na nikaokolewa kutoka katika mdomo wa simba.
18Bwana ataniokoa kutokana na kila mashambulizi maovu na atanileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Utukufu uwe wake milele na milele. Amina.
19Msalimu Priska na Akila na wale wa nyumbani mwake Onesiforo.
20Erasto alibaki Korintho. Nilimwacha Trofimo kule Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa.
21Jitahidi kuja kabla ya msimu wa baridi.
Ebulo anakusalimu, na Pude, Lino, na Klaudia, na ndugu na dada wote.
22Bwana awe nawe. Neema ya Mungu iwe nanyi.