Ufunuo 10

Ufunuo 10

Malaika Na Kitabu kidogo

1Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni akiwa amevikwa wingu na upinde wa mvua ulizunguka kichwa chake. Uso wake ulikuwa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.

2Malaika alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichofunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na mguu wa kushoto nchi kavu.

3Alipaza sauti yake kama simba anavyounguruma na sauti za radi saba zikasikika.

4Radi saba ziliongea, na nikaanza kuandika. Lakini nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Usiandike ambacho radi saba zinasema. Yaache mambo hayo yawe siri.”

5Kisha nikamwona malaika aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu akinyoosha mkono wake kuelekea mbinguni.

6Malaika akaapa kwa nguvu ya yule aishiye milele na milele. Ndiye aliyeziumba mbingu na vyote vilivyomo ndani yake. Aliumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, na aliumba bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Malaika alisema, “Hakutakuwa kusubiri tena!

7Katika siku ambazo malaika wa saba atakuwa tayari kupuliza tarumbeta yake, mpango wa siri wa Mungu utakamilika, nao ni Habari Njema ambayo Mungu aliwaambia watumishi wake, manabii.”

8Kisha nikasikia tena sauti ile ile kutoka mbinguni. Ikaniambia, “Nenda ukachukue kitabu kilicho wazi mkononi mwa malaika, aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu.”

9Hivyo nilimwendea malaika nikamwomba anipe kitabu kidogo. Naye aliniambia, “Chukua kitabu na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako lakini kitakuwa kitamu kama asali mdomoni mwako.”

10Hivyo nilichukua kitabu kidogo kutoka mkononi mwa malaika na kukila. Mdomoni mwangu kilikuwa na ladha tamu kama asali, lakini baada ya kukila, kilikuwa kichungu tumboni mwangu.

11Kisha nikaambiwa, “Ni lazima uwatabirie tena watu wa asili tofauti, mataifa, lugha na watawala.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International