Amosi 3

Amosi 3

1Enyi Waisraeli, sikilizeni neno Mwenyezi-Mungu alilosema dhidi yenu, enyi taifa zima alilolitoa nchini Misri:

2“Kati ya mataifa yote ulimwenguni,

ni nyinyi tu niliowachagua.

Kwa hiyo nitawaadhibu nyinyi,

kwa sababu ya uovu wenu wote.”

Jukumu la nabii

3Je, watu wawili huanza safari pamoja,

bila ya kufanya mpango pamoja kwanza?

4Je, simba hunguruma porini

kama hajapata mawindo?

Je, mwanasimba hunguruma pangoni mwake

kama hajakamata kitu?

5Je, mtego bila chambo

utamnasa ndege?

Je, mtego hufyatuka

bila kuguswa na kitu?

6Je, baragumu ya vita hulia mjini

bila kutia watu hofu?

Je, mji hupatwa na janga

asilolileta Mungu?

7Hakika, Bwana Mwenyezi-Mungu hafanyi kitu

bila kuwafunulia watumishi wake manabii nia yake.

8Simba akinguruma,

ni nani asiyeogopa?

Bwana Mwenyezi-Mungu akinena,

ni nani atakataa kuutangaza ujumbe wake?

Kuangamizwa kwa Samaria

9Tangazeni katika ikulu za Ashdodi,

na katika ikulu za nchi ya Misri:

“Kusanyikeni kwenye milima

inayoizunguka nchi ya Samaria,

mkajionee msukosuko mkubwa

na dhuluma zinazofanyika humo.”

10Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Watu hawa wameyajaza majumba yao

vitu vya wizi na unyang'anyi.

Hawajui kabisa kutenda yaliyo sawa!

11Kwa hiyo, adui ataizingira nchi yao,

atapaharibu mahali pao pa kujihami,

na kuziteka nyara ikulu zao.”

12Mwenyezi-Mungu, asema hivi: “Kama vile mchungaji ampokonyavyo simba kinywani miguu miwili tu au kipande cha sikio la kondoo, ndivyo watakavyonusurika watu wachache tu wa Israeli wakaao Samaria, ambao sasa wanalalia vitanda vizuri na matandiko ya hariri.”[#3:12 Maana katika Kiebrania si dhahiri.]

13Bwana Mungu wa majeshi asema hivi:

“Sikilizeni, mkawaonye wazawa wa Yakobo:

14Siku nitakapowaadhibu Waisraeli

kwa sababu ya makosa yao,

nitayaharibu pia madhabahu ya mji wa Betheli.

Nitazikata pembe za kila madhabahu

na kuziangusha chini.

15Nitaziharibu nyumba zote mjini na vijijini;

nitazibomoa nyumba zilizopambwa kwa pembe,

majumba makubwamakubwa hayatasalia hata moja.

Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania