Mhubiri 11

Mhubiri 11

Afanyavyo mwenye busara

1Jishughulishe na biashara

hata kama kwa kubahatisha;

yawezekana baadaye

ukapata chochote kile.

2Wagawie watu saba hata wanane sehemu yako,

maana, hujui balaa litakalofika duniani.

3Mawingu yakijaa maji, mvua hunyesha;

mti ukiangukia kusini au kaskazini,

hapo uangukiapo ndipo ulalapo.

4Anayengoja upepo hatapanda mbegu,

anayesubiri mawingu yatoweke, hatavuna kitu.

5Usivyojua jinsi uhai unavyoingia katika mifupa ya mtoto tumboni mwa mamake, kadhalika huwezi kuelewa matendo ya Mungu, ambayo hufanya kila kitu.[#11:5 au roho iingiavyo katika mimba tumboni mwa mja mzito.]

6Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri.

7Mwanga wafaa, na kuliona jua kwapendeza macho.

8Mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie miaka hiyo yote; lakini akumbuke kuwa siku za giza zitakuwa nyingi, na kwamba yote yatakayofuata ni bure.

Mawaidha kwa vijana

9Ewe kijana, furahia ujana wako, moyo wako, uchangamke wakati ungali kijana. Fuata mapenzi ya moyo wako na upeo wa macho yako. Lakini kumbuka kwamba Mungu atakuhukumu kadiri ya hayo yote.

10Ondoa mahangaiko moyoni mwako, jikinge, usipate maumivu mwilini kwa sababu ujana na mwisho wa maisha ni bure kabisa.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania