Yoshua 14

Yoshua 14

Kugawanywa kwa nchi ya Kanaani

1Yafuatayo ni maeneo ya nchi ambayo walipewa Waisraeli katika nchi ya Kanaani. Kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, pamoja na wakuu wa koo za makabila ya Waisraeli waliwagawia Waisraeli.

2Sehemu yao hiyo waligawiwa kwa kura kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose awape yale makabila tisa na nusu.[#Taz Hes 26:52-56; 34:13]

3Mose alikuwa ameyapa yale makabila mawili na nusu sehemu yao mashariki ya Yordani, lakini Walawi hawakuwa wamepewa sehemu yao pamoja nao.[#Taz Hes 32:33; 34:14-15; Kumb 3:12-17]

4Wazawa wa Yosefu walikuwa makabila mawili: Manase na Efraimu. Kabila la Lawi halikupewa sehemu yoyote ya nchi, ila miji tu ya kuishi na sehemu za malisho kwa ajili ya wanyama wao na riziki zao.

5Basi, Waisraeli wakaigawanya nchi kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Kalebu anapewa mji wa Hebroni

6Siku moja watu wa kabila la Yuda walimwendea Yoshua huko Gilgali. Kalebu mwana wa Yefune, ambaye alikuwa Mkenizi, akamwambia Yoshua, “Bila shaka unakumbuka jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, mtu wa Mungu, juu yangu na wewe tulipokuwa Kadesh-barnea:[#Taz Hes 14:30]

7Nilipokuwa na umri wa miaka arubaini, Mose mtumishi wa Mungu, alinituma kutoka Kadesh-barnea, kwenda kuipeleleza nchi. Niliporudi nilimletea habari za mambo ya huko kadiri nilivyoamini moyoni mwangu,[#Taz Hes 13:1-30]

8hali wale wenzangu waliokwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo, lakini mimi nilimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kwa uaminifu.

9Siku hiyo Mose aliniapia, ‘Hakika sehemu ya nchi ile ambayo ulipita itakuwa yako wewe na wazawa wako milele. Kwa sababu ya uaminifu wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako’.[#Taz Hes 14:24]

10Lakini sasa tazama! Ni muda wa miaka arubaini na mitano tangu Mwenyezi-Mungu alipoongea na Mose, wakati Waisraeli walipokuwa wanapitia jangwani. Tangu wakati huo Mwenyezi-Mungu, kama alivyoahidi, amenihifadhi hai mpaka leo, na sasa mimi nina umri wa miaka themanini na mitano.

11Lakini bado nina nguvu kama nilivyokuwa wakati ule Mose aliponituma. Hata sasa nina nguvu za kuweza kupigana vita au kufanya kazi nyingine yoyote.

12Sasa naomba unipe nchi hii ya milima ambayo Mwenyezi-Mungu aliniahidi siku ile. Wewe ulisikia siku ile kwamba Waanaki waliishi humo katika miji yenye ngome; huenda Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.”

13Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune na kumpa mji wa Hebroni kuwa sehemu yake.

14Kwa hiyo, mji wa Hebroni ni sehemu yao wazawa wa Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi mpaka hivi leo, kwa sababu Kalebu alikuwa mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

15Mji wa Hebroni hapo awali uliitwa Kiriath-arba. Arba alikuwa mtu maarufu kuliko wote kati ya Waanaki. Nchi nzima ikawa tulivu bila vita.[#14:15 Maana yake mji wa Arba.]

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania