The chat will start when you send the first message.
1Heri mtu asiyefuata shauri la waovu,
asiyeshiriki njia za wenye dhambi,
wala kujumuika na wenye dharau;
2bali huifurahia sheria ya Mwenyezi-Mungu,
na kuitafakari mchana na usiku.
3Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito,
unaozaa matunda kwa wakati wake,
na majani yake hayanyauki.
Kila afanyalo hufanikiwa.
4Lakini waovu sivyo walivyo;
wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5Kwa hiyo watu waovu wataanguka wakati wa hukumu,
wenye dhambi hawatakaa na kusanyiko la waadilifu.
6Maana Mwenyezi-Mungu huziongoza njia za waadilifu;
lakini njia za waovu zitaishia katika maangamizi.