Zaburi 145

Zaburi 145

Wimbo wa kumsifu Mungu

1Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu;

nitalitukuza jina lako daima na milele.

2Nitakutukuza kila siku;

nitalisifu jina lako daima na milele.

3Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi;

ukuu wake hauwezi kuchunguzika.

4Kizazi hata kizazi, sifa za matendo yako zitasimuliwa,

watu watatangaza matendo yako makuu.

5Nitanena juu ya utukufu na fahari yako,

nitayatafakari matendo yako ya ajabu.

6Watu watatangaza ukuu wa matendo yako ya ajabu,

nami nitatangaza ukuu wako.

7Watatangaza sifa za wema wako mwingi,

na kuimba juu ya uadilifu wako.

8Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema;

hakasiriki ovyo, amejaa fadhili.

9Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote,

ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote.

10Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu,

nao waaminifu wako watakutukuza.

11Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako,

na kutangaza juu ya nguvu yako kuu,

12ili kila mtu ajue matendo yako makuu,

na fahari tukufu ya ufalme wako.

13Ufalme wako ni ufalme wa milele;

mamlaka yako yadumu vizazi vyote.

Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote,

ni mwema katika matendo yake yote.

14Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka;

huwainua wote waliokandamizwa.

15Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu,

nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake.

16Waufumbua mkono wako kwa ukarimu,

watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai.

17Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote;

ni mwema katika matendo yake yote.

18Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba,

wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu.

19Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha;

husikia kilio chao na kuwaokoa.

20Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda;

lakini atawaangamiza waovu wote.

21Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu;

viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu,

milele na milele.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania