The chat will start when you send the first message.
1Mungu anajulikana katika Yuda;
jina lake ni kuu katika Israeli.
2Makao yake yamo huko Salemu;[#76:2 Jina la zamani la Yerusalemu.]
maskani yake huko Siyoni.
3Huko alivunja mishale ya adui;
alivunja ngao, panga na silaha za vita.
4Wewe, ee Mungu, watukuka mno;
umejaa fahari kuliko milima ya milele.
5Wenye nguvu walipokonywa nyara zao,
sasa wamelala usingizi wa kifo,
mashujaa wa vita hawakuweza kutumia mikono yao.
6Ulipowakemea, ee Mungu wa Yakobo,
farasi na wapandafarasi walikufa ganzi.
7Wewe, ee Mungu, ni wa kutisha mno!
Nani awezaye kustahimili mbele yako ukikasirika?
8Ulijulisha hukumu yako toka mbinguni;
dunia iliogopa na kunyamaza;
9wakati ulipoinuka kutekeleza hukumu,
kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.
10Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako;
na waliookoka vitani watafanya sikukuu zako.
11Mtimizieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ahadi zenu;
enyi mlio karibu mpeni zawadi Mungu wa kutisha.
12Yeye huzitoa roho za wakuu;
huwatisha wafalme wa dunia.