Zaburi 90

Zaburi 90

KITABU CHA NNE

Mungu wa milele na binadamu kiumbe

1Ee Bwana, tangu vizazi vyote,

wewe umekuwa usalama wetu.

2Kabla ya kuwapo milima,

kabla hujauumba ulimwengu;

wewe ndiwe Mungu, milele na milele.

3Wamwambia binadamu, “Rudi mavumbini!”

Naye binadamu hurudi mavumbini alimotoka!

4Kwako miaka elfu ni kama siku moja tu,[#Taz 2Pet 3:8]

ni kama jana ambayo imekwisha pita;

kwako ni kama mkesha mmoja wa usiku!

5Wawafutilia mbali watu kama ndoto!

Binadamu ni kama nyasi zinazochipua asubuhi:

6Asubuhi huchipua na kuchanua,

jioni zimekwisha nyauka na kukauka.

7Hasira yako inatuangamiza;

tunatishwa na ghadhabu yako.

8Maovu yetu umeyaweka mbele yako;

dhambi zetu za siri ziko wazi mbele yako.

9Kwa hasira yako maisha yetu yatoweka,

yanaisha kama pumzi.

10Miaka ya kuishi ni sabini,

au tukiwa wenye afya, themanini;

lakini yote ni shida na taabu!

Siku zapita mbio, nasi twatoweka mara!

11Nani anayetambua uzito wa hasira yako?

Nani anayejali matokeo ya ghadhabu yako?

12Utufundishe ufupi wa maisha yetu

ili tuweze kuwa na hekima.

13Urudi, ee Mwenyezi-Mungu!

Utakasirika hata lini?

Utuonee huruma sisi watumishi wako.

14Utushibishe fadhili zako asubuhi,

tushangilie na kufurahi maisha yetu yote.

15Utujalie sasa miaka mingi ya furaha,

kama ulivyotupa miaka mingi ya shida na taabu.

16Utuoneshe matendo yako sisi watumishi wako;

uwaoneshe wazawa wetu uwezo wako mtukufu.

17Utufadhili ee Bwana, Mungu wetu;

uzitegemeze kazi zetu,

uzifanikishe shughuli zetu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania