The chat will start when you send the first message.
1Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine?
2Nyinyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma.
3Ni dhahiri kwamba nyinyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu.[#3:3 Hapa pana mlinganuo muhimu sana ambao umetoka katika A.K. Rejea Kut 24:12; na Yer 31:33 (aya ambayo imenukuliwa pia katika Ebr 10:16). Yamkini hapa Paulo anadokeza tofauti kati ya agano la kale na lile agano jipya, wazo ambalo ataliendeleza zaidi kuanzia aya ya 6.]
4Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo.
5Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu:
6maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uhai.
7Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mng'ao wake. Tena mng'ao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho,[#3:7 Maneno haya mawili yanatumika kutafsiri neno lile lile moja la Kigiriki “doksa”. Wakati Mose aliposhuka kutoka Mlima Sinai akiwa na zile Amri Kumi uso wake ulikuwa unang'ara kwa sababu ya utukufu wa Mungu.; #3:7-11 Katika aya hizi kuna mlinganuo baina ya sheria ya Mose na agano jipya (mtindo wa mlinganuo ambao unatumiwa pia na Yesu katika Luka 11:13; 12:24-28 na Paulo katika Rom 5:9-10; 11:12,24; 1Kor 6:3). Hoja ya Paulo ina msingi wake katika Kut 34:29-35.]
8basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi.
9Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma iletayo uadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi.[#3:9 Rejea Kumb 27:26. Sheria ambayo ilitumika kuwahukumu watu inabainishwa na ujumbe ulio na utukufu zaidi ambao kwao Mungu anatufanya waadilifu (Rom 3:21-22).]
10Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka.
11Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi.
12Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu.
13Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mng'ao ule uliokuwa unafifia.[#3:13 Hapa Paulo anaona kwamba kitambaa kilichotumika kuufunika uso wa Mose kilikuwa na shabaha ya kuuficha mng'ao huo (Kut 34:29-35). Lakini katika aya 14-16 Paulo anaendeleza picha hiyo ya msingi hata kuifanya ijumuishe kile ambacho kiliwazuia na kinaendelea kuwazuia Wayahudi wasitambue hali ya mpito ya sheria ya Mose. Ling Rom 11:7-8,25.]
14Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo.[#3:14 Yaani Maandiko ya Biblia ya Kiebrania.; #3:14 Tafsiri nyingine yamkini: “Maana hawakupata kufunuliwa kwamba agano hilo lilibatilishwa na Kristo”.]
15Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo sheria akili zao huwa zimefunikwa.
16Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa.[#3:16 Tafsiri nyingine yamkini: “Lakini wakati (Mose) anapomgeukia Bwana huondoa kile kifuniko” (Kut 34:34). Katika tafsiri hii ya pili Mose ndiye anayehusika; katika ile ya kwanza ni mtu yeyote hata Mose na “Bwana” ni Kristo.]
17Hapa “Bwana” ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru.[#3:17 Baadhi hufafanua kwamba hapa panadhihirisha umoja wa ndani kabisa baina ya “Roho Mtakatifu” na “Bwana”, ambapo hapa “Bwana” ni Mungu au Yesu Kristo. Wengine wanafikiri kuwa “Bwana” anayetajwa katika Kut 34:34 ni Roho Mtakatifu.]
18Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, tunaona kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.[#3:18 Tafsiri nyingine: “Twaonesha kama katika kioo, utukufu wa Bwana”. Kadiri ya mlinganuo wa sehemu hii inaonekana kuwa tafsiri ya “twaona” kama katika kioo inaafiki hapa kuliko “tunaonesha” au “tunarudisha” kama katika kioo. Kwa hiyo jambo linalolinganishwa hapo awali: Waisraeli (na Mose) kwa upande mmoja na Wakristo (na Paulo) kwa upande mwingine ni hali ya “kufunikwa” kwa akili zao Waisraeli wasione hali ya mpito wa sheria ya Mose, na hali ya “kutofunikwa” kwa Wakristo ambao sasa wanaona wazi utukufu wa kudumu wa Kristo, kwa msaada wa Roho.]