2 Wakorintho 6

2 Wakorintho 6

1Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure.

2Mungu asema hivi:

“Wakati wa kufaa nimekusikiliza,

wakati wa wokovu nikakusaidia.”

Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu!

3Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuizi chochote.

4Badala yake, tunajionesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.[#6:4-5 Paulo anataja visa vingine ambavyo alipata taabu, akafarijiwa katika shughuli zake za kuhubiri Habari Njema ya Yesu; rejea 2Kor 11:23-27.]

5Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula.

6Tunajionesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,

7kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu kila upande.[#6:7 Neno kwa neno: “… silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto”. Katika vita nyakati hizo za kale mtu alishika upanga au mkuki kwa mkono wa kulia kupigana na kwa mkono wa kushoto kujikinga. Kwa hiyo tafsiri nyingine kulingana na maelezo hayo yaweza kuwa: Silaha yetu ya kushambulia na kujikinga ni uadilifu. Tazama pia matumizi ya lugha ya silaha kueleza maadili ya kiroho Efe 6:10-17 na ushindi juu ya uovu (10:4; Rom 13:12,14; Efe 6:10-17; Fil 1:30; 2:25; 1Tim 1:18; 2Tim 2:3-4; File 2).]

8Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli;

9kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote; kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni hai kabisa.

10Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini, twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.

11Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa.

12Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu nyinyi wenyewe, na si kwa upande wetu.

13Sasa nasema nanyi kama watoto wangu: wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.

Onyo kuhusu mitindo ya watu wasiomjua Mungu

14Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja?

15Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Mwaamini ana uhusiano gani na asiyeamini?[#6:15 Kigiriki kina “Beliar” ambalo Kiebrania ni “Beliali” neno lenye maana “Mwovu” au “Bure”.]

16Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema:[#6:16 1Kor 3:16; 6:19; Efe 2:20-21.; #6:16 Lawi 26:12; Yer 32:38; Eze 37:27.]

“Nitafanya makao yangu kwao,

na kuishi kati yao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.”

17Kwa hiyo Bwana asema pia:[#6:17 Isa 52:11.]

“Ondokeni kati yao,

mkajitenge nao;

msiguse kitu najisi,

nami nitawapokea.

18Mimi nitakuwa Baba yenu,

nanyi mtakuwa wanangu, waume kwa wake,

asema Bwana Mwenye Nguvu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania