The chat will start when you send the first message.
1Yafuatayo ni maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, aliyekuwa mfalme huko Yerusalemu.[#1:1 Taz pia 1:12. Jina hili la sifa linatafsiri kile tulicho nacho katika Kiebrania kama “Kohelethi”, neno ambalo lina uhusiano na “kahal” kanisa (“eklesiastes” katika tafsiri ya Kigiriki).]
2Bure kabisa, bure kabisa,[#1:2 Maneno haya yanatafsiri msemo wa Kiebrania ambao una maana ya kitu ambacho hakina maana, si cha kudumu na hakina sababu ya kuweko, kama vile ndoto au pumzi Kiebrania “hebel” - pumzi ya binadamu hutoweka upesi na haidumu. Wazo hilo linatiliwa mkazo kwa kuonesha undani wa hali ya binadamu wa kupita tu hapa duniani, wazo ambalo linapatikana pia katika Zab 62:9. Kutokana na mtindo huo, inawezekana kutafsiri pia kama: “Kila kitu hakifai, hakifai kabisa!”]
nakuambia mimi Mhubiri!
Kila kitu ni bure kabisa!
3Binadamu hufaidi nini[#1:3 Hili ni swali lisilodai majibu. Lengo la maswali ya mtindo huu ni kusisitiza jambo na kuliimarisha. Mwandishi anarudia wazo hilo; yaani mambo anayotenda binadamu, hata yale ya kuwaza na kuwazua ni ya bure, hayafai kabisa (2:22), na yeye mwandishi mwenyewe, hekima yake haifai kitu (1:16-12; 2:1).]
kwa jasho lake lote hapa duniani?
4Kizazi chapita na kingine chaja,
lakini dunia yadumu daima.
5Jua lachomoza na kutua;
laharakisha kwenda machweoni.
6Upepo wavuma kusini,
wazunguka hadi kaskazini.
Wavuma na kuvuma tena,
warudia mzunguko wake daima.
7Mito yote hutiririkia baharini,
lakini bahari kamwe haijai;
huko ambako mito hutiririkia
ndiko huko inakotoka tena.
8Mambo yote husababisha uchovu,
uchovu mkubwa usioelezeka.
Jicho halichoki kuona,
wala sikio kusikia.
9Yaliyokuwako ndio yatakayokuwako,
yaliyotendeka ndio yatakayotendeka;
duniani hakuna jambo jipya.
10Watu husema, “Tazama jambo jipya,”
kumbe lilikwisha kuwako zama za kale.
11Hakuna mtu anayekumbuka ya zamani[#1:8-11 Wengine wanafikiri mwandishi anaona kuwa mambo hayo yanasababisha uchovu na kukinaisha kutokana na kurudiarudia kwake kwa sababu ameshindwa kufahamu mpango wa Mungu. Hata hivyo katika 3:11 mwandishi anaamini kwamba Mungu hufanya kila kitu kitukie kwa wakati wake alioupanga tangu zama za kale. Kwa hiyo mwandishi anajiona hawezi kitu.]
wala atakayekumbuka yatakayotukia baadaye.
12Mimi Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli, huko Yerusalemu.[#1:12 Taz utangulizi kwa kitabu hiki cha Mhubiri. Katika sehemu hii vitu ambavyo vilisemwa juu ya Solomoni katika vitabu vya Wafalme vinarudiwa. Kuhusu hekima yake (1:16), taz 1Fal 4:29-31; kuhusu utajiri wake (2:4-8) taz 1Fal 10:10,14-22,23-27, n.k. Katika Meth 1:16-17 msomaji hataacha kumfikiria Solomoni wakati anafuata wazo linalotolewa katika aya hizo. Si ajabu basi kwamba wengi walifikiri Solomoni ndiye aliyekuwa mwandishi wa kitabu hiki.]
13Nilipania kuchunguza na kutafuta kwa hekima kila kitu kinachotukia duniani. Hiyo ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu.
14Nimeyaona yote yanayofanywa duniani; yote ni bure: ni sawa na kufukuza upepo![#1:13-14 “Nilipania”, au, neno kwa neno: “Niliutia moyo wangu”, neno “moyo” likitumika katika maana yake ya kikao cha mawazo na maamuzi ya binadamu kulingana na utamaduni wa lugha ya Waebrania (na pia kwa Waswahili – moyo ni kikao cha mawazo, uamuzi, n.k.). Fungu la maneno “kufukuza upepo” ni msemo ulioongezwa katika ule wa kawaida: “Bure kabisa, bure kabisa” ili kutilia mkazo zaidi wazo hilo hilo. Tafsiri nyingine yamkini: “ni sawa na kukimbizana na upepo” au, “ni shughuli ya bure” (2:11,17,26; 4:4,6; 6:9).]
15Kilichopindika hakiwezi kunyoshwa,
kisichokuwapo hakiwezi kuhesabiwa.
16Basi, nikatafakari nikisema, “Nimejipatia hekima nyingi zaidi kupita wote waliopata kutawala Yerusalemu kabla yangu. Naam, nina uzoefu wa hekima na maarifa.”[#1:16-17 Mwandishi wa kitabu hiki anachunguza yanayomwafiki yeye binafsi na maamuzi anayotoa kuhusu la kufanya, lakini anagundua ukweli wake (taz pia 2:1-2).]
17Nilipania kubainisha kati ya hekima, wazimu na upumbavu. Lakini niligundua kwamba kufanya hivyo ni sawa na kufukuza upepo.
18Maana katika kuwa na hekima nyingi mna wasiwasi;
na aongezaye maarifa zaidi huongeza huzuni zaidi.