Mathayo 11

Mathayo 11

Ujumbe kutoka kwa Yohane Mbatizaji

(Luka 7:18-35)

1Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.[#11:1 Taz maelezo ya Mat 7:28.]

2Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake,[#11:2 Mat 4:12 maelezo.; #11:2 Wanafunzi au wafuasi wa Yohane Mbatizaji wanatajwa mara kadhaa katika Agano Jipya; taz Mat 9:14; Luka 11:1; Yoh 1:35; 3:25.]

3wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?”

4Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona:

5vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema.[#11:5 Taz Isa 19:18-19; 26:19; 35:5-6; 42:7,18; 61:1.]

6Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami.”[#11:6 Au “asiyeniona mimi kuwa kizuizi” (cha kuamini).]

7Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?

8Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme.

9Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.

10“Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu:

‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie,

ambaye atakutayarishia njia yako’.

11Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye.[#11:11 Yeye, kama inavyoonekana, hakuwa mtu wa kawaida. Kama mtangulizi wa Masiha (3:1-15; rejea Mal 3:1), ni yeye tu miongoni mwa binadamu ambaye alimkaribia Masiha zaidi kwa ukuu. Huduma yake ilimalizia kipindi kile cha kwanza cha manabii na Sheria ya Mose (11:13). Yeye hakuwa wa kipindi kipya cha utawala wa Mungu.]

12Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu.[#11:12 Msemo huu ni mgumu kuuelewa (Luka 16:16). Baadhi wanafikiri watu wakali ni wale waliokuwa wakiupinga utawala wa Mungu kama Herode na kuwatesa waumini. Wengine wanafikiri yahusu utawala wa Mungu ambao unaenea kwa nguvu isiyoweza kuzuiwa. Rejea Luka 16:16.]

13Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi.

14Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja.[#11:14 Yaani ndiye Mtangulizi wa Masiha (Mal 4:5; Mat 17:10-13; Marko 9:11-13; Luka 1:17).]

15Mwenye masikio na asikie!

16“Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine:[#11:16-17 Picha ya watoto wanaocheza lakini hawakubaliani wao kwa wao inatumika hapa kuonesha kwamba watu hawafanyi kile ambacho wangalipaswa kufanya.]

17‘Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza!

Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkuomboleza!’

18Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: ‘Amepagawa na pepo’.

19Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: ‘Mwangalieni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.”

Miji isiyoamini

(Luka 10:13-15)

20Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu:

21“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu.[#11:21 Neno hilo lamaanisha lawama au hata apizo na sio onyo tu (taz 23:13).]

22Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni.

23Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo.[#11:23 Rejea Isa 14:13-15.]

24Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.”[#11:24 10:15; Luka 10:12.]

Njoni kwangu mpumzike

(Luka 10:21-22)

25Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo.[#11:25 Yaani viongozi wa dini ambao hawakuupokea ujumbe wa ufalme wa Mungu.; #11:25 Yaani wanafunzi wake Yesu ambao waliupokea ujumbe wake.]

26Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza.

27“Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia.[#11:27 Mat 28:18: Yoh 3:35; 13:3; 17:2.; #11:27 Maneno haya yagusia pia uhusiano wa pekee ulioko kati ya Mwana yaani Yesu na Mungu Baba yake. Taz Yoh 1:18; 6:65; 10:14-15.]

28Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu.[#11:29 Hapa neno “nira” linatumiwa kwa maana ya mafundisho ya mwalimu. Rejea Mat 23:2-4; Luka 11:46.]

30Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania