Mathayo 22

Mathayo 22

Mfano wa karamu ya harusi

(Luka 14:15-24)

1Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano:

2“Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi.[#22:2 Katika Kigiriki ni wingi labda kwa kuwa sherehe ya harusi ilidumu kwa siku kadhaa. Mfano wa harusi katika Biblia unatumiwa pengine kuelezea uhusiano na muungano wa furaha wa Mungu na watu wake (taz Mat 25:1-12). Kilele cha mfano huu kinachotiliwa mkazo si huyo mwana wa mfalme bali kule kukataa kwa wale walioalikwa kwanza.]

3Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika.

4Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’

5Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake,

6na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua.

7Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao.

8Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili.

9Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’

10Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni.[#22:10 Yaani watu wote wanaitwa. Mwaliko huo unapelekwa kwa kila mtu, lakini yapo pia mambo yanayotakiwa kwao (aya 11). Angalia jinsi mfano huu unavyofanana na ile mifano ya Mat 13:24-30,36-43,47-50.]

11“Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi.

12Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya.

13Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’”[#22:13 Taz maelezo ya 8:12; rejea pia 25:30 na Luka 13:28.]

14Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.”[#22:11-14 Aya 11-14 za mfano huu wa Mathayo hazina sambamba zake katika ule mfano sambamba wa Luka 14:15-24.]

Kulipa kodi kwa Kaisari

(Marko 12:13-17; Luka 20:20-26)

15Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake.

16Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako.[#22:16 Marko 3:6. Kikundi hicho kilikuwa cha watu waliomuunga mkono Herode Antipa na ukoo wa kifalme ulioanzishwa na Herode Mkuu.; #22:16 Yaani, njia aliyoonesha Mungu au njia ya kwenda kwa Mungu.]

17Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?”

18Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu?[#22:18 Kama Yesu angesema Wayahudi wasilipe kodi angeshtakiwa kwa kosa la uhaini; na kama angesema ni lazima walipe, wananchi wenzake, yaani Wayahudi, wangemshutumu kuwa msaliti.]

19Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha.

20Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?”

21Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.”[#22:21 Rom 13:6-7; taz pia 1Pet 2:13-17.]

22Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.

Suala juu ya ufufuo

(Marko 12:18-27; Luka 20:27-40)

23Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu.

24Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto.[#22:24 Desturi hii ambayo msingi wake ni Kumb 25:5-10 (lakini taz Lawi 18:16; 20:21) ilikuwa na lengo la kuendeleza ukoo na kuhalalisha urithi. Desturi hii ilijulikana pia kwa mataifa mengine ya kale kama vile Wahiti na Waasiria.]

25Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane.

26Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba.

27Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama.

28Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.”[#22:28 Kisa walichosema hao Masadukayo ni kisa cha kubuni kusudi waoneshe kama walivyoamini wao kwamba kufufuliwa watu na kuishi tena ni wazo la kipumbavu.]

29Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu.

30Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni.

31Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia,

32‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”[#22:32 Jibu la Yesu lina sehemu mbili: (i) Uwezo na nguvu ya Mungu itawabadili watu na uhai mpya watakaopata hautakuwa kama ule wa kwanza. (ii) Maneno ya Kut 3:6 ni ushahidi kwamba mababu Abrahamu, Isaka na Yakobo wako hai, kwani Mungu alisema yeye ni Mungu wao (na sio Mungu wa wafu).]

33Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.

Amri kuu

(Marko 12:28-34; Luka 10:25-28)

34Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja.

35Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu,

36“Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?”[#22:36 Taz maelezo katika Marko 12:28.]

37Yesu akamjibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’.

38Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza.

39Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’.[#22:39 Au “ni muhimu”; kufanana huko si kwa maneno bali kwa umuhimu wake.]

40Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.”

Suala juu ya Kristo

(Marko 12:35-37; Luka 20:41-44)

41Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza,

42“Nyinyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Wa Daudi.”[#22:42 Wayahudi waliamini kwamba Masiha angekuwa wa ukoo au mzawa wa Daudi; taz k.m. Marko 12:35 maelezo.]

43Yesu akawaambia, “Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema:

44‘Bwana alimwambia Bwana wangu:

keti upande wangu wa kulia,

mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’

45Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo ‘Bwana,’ anawezaje kuwa mwanawe?”

46Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania