The chat will start when you send the first message.
1Yesu alitoka hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonesha majengo ya hekalu.[#24:1—25:46 Sehemu hii ni simulizi kuu la tano la Yesu nalo lahusu mwisho wa nyakati (sura 24—25); taz Utangulizi wa Injili ya Mathayo.]
2Yesu akawaambia, “Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.”[#24:2 Hekalu la Yerusalemu liliteketezwa na majeshi ya Waroma mwaka 70 B.K. (rejea Luka 19:44). Majeshi hayo yaliongozwa na mtawala Tito, mtawala wa Kiroma.]
3Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?”[#24:3 Katika Marko ni Petro, Yakobo na Yohane.; #24:3 Matukio hayo mawili yanaonekana kuwa na uhusiano; kuja kwa Mwana wa Mtu kutakuwa ishara ya mwisho wa historia ya binadamu.]
4Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
5Maana wengi watatokea wakisema kila mmoja kwamba yeye ndiye Kristo nao watawapotosha watu wengi.[#24:5 1Yoh 2:18.]
6Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
7Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.
8Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.
9“Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa sababu ya jina langu.
10Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.
11Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.
12Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.
13Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.
14Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.
15“Basi, mtakapoona ‘Chukizo Haribifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),[#24:15 Picha iliyotolewa kutoka Dan 9:27; 11:31; 12:11. Matumizi ya msemo huu hapa ni hasa kuhusu kuteketezwa kwa mji wa Yerusalemu na hekalu kutiwa unajisi mwaka wa 70 B.K., taz Luka 21:20.; #24:15 Labda haya ni maneno ya ilani kwa Wakristo kwa vile aya hii ilikuwa na maana iliyofichika kwa watu wa nje.]
16hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.
17Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake.[#24:17 Taz pia Luka 17:31. Maagizo na maonyo katika sehemu hii ya 24:15-22 yanazungumzia juu ya wakati ambapo majeshi yatavamia Yerusalemu (Luka 21:20-24). Mapaa ya nyumba za wakati huo yalikuwa yamewekwa ubapa na watu waliweza kwenda huko kwa ngazi upande wa nje wa nyumba.]
18Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
19Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
20Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato!
21Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena.
22Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa.
23“Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: ‘Kristo yuko hapa’ au ‘Yuko pale,’ msimsadiki.
24Maana watatokea akina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu.
25Sikilizeni, nimekwisha waonya kabla ya wakati.
26Basi, wakiwaambieni, ‘Tazameni, yuko jangwani,’ msiende huko; au, ‘Tazameni, amejificha ndani,’ msisadiki;[#24:26-27 Aya hizi ni sambamba na Luka 17:23-24; na 24:28 ni sambamba na Luka 17:37.]
27maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
28Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
29“Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.[#24:29 Lugha inayotumiwa hapa inachukua picha kutoka Agano la Kale. Taz Isa 13:10; Eze 32:7; Yoeli 2:10,31; 3:15; Ufu 6:12.; #24:29 Taz Isa 34:4; Ufu 6:13.; #24:29 Nguvu za angani ambazo ilisadikiwa kumiliki nyota na sayari.]
30Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.[#24:30: Tazama Dan 7:13; Zek 12:10-14; Rev 1:7.]
31Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.
32“Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia.
33Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.
34Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.[#24:34 Hayo mambo yaliyotajwa katika aya zilizotangulia yangetukia wakati wasikilizaji wake Yesu wakiwa bado hai (16:28).]
35Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
36“Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.[#24:36 Hati nyingine za kale hazina maneno haya.]
37Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
38Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.
39Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.
40Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
41Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.
43Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.[#24:43 Kuhusu 24:43-44, taz Luka 12:39-40. Onyo la namna hiyohiyo liko katika 1Thes 5:2 na Ufu 3:3.]
44Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”
45Yesu akaendelea kusema, “Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake?
46Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.
47Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote.
48Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia kurudi,’
49kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi,
50bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua.
51Atamwadhibu vibaya na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.[#24:51 Neno kwa neno: atamkata vipandevipande. Maana yake yawezekana kuwa “atamwadhibu vikali” au “atamtenga mbali.”; #24:51 Taz Mat 8:12 maelezo.]