The chat will start when you send the first message.
1Yesu aliposhuka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata.[#8:1—9:38 Sehemu hii ya simulizi ambayo sasa iko katikati ya mahubiri mawili ina miujiza kumi ya Yesu pamoja na masimulizi mengine.]
2Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia na kusema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!”[#8:2 Ugonjwa wa ukoma ulifikiriwa na Wayahudi kusababisha unajisi, yaani kumfanya mtu kuwa mwiko kuhusu mambo ya kidini; vilevile kila aliyemgusa mkoma alikuwa pia najisi (Lawi 5:3). Hata hivyo, Yesu alinyosha mkono, akamgusa, akamponya.]
3Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika.” Mara huyo mtu akapona ukoma wake.
4Kisha Yesu akamwambia, “Angalia, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani, na kutoa sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”[#8:4 Rejea Mat 9:30; 12:16. “Usimwambie mtu yeyote”. Kuhusu jambo hilo la kuwakataza wanafunzi wake wasiwaambie watu juu ya miujiza ya Yesu, taz Marko 1:34.; #8:4 Taz Lawi 14:1-32.]
5Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi[#8:5 Au kamanda wa jeshi. Kwa kawaida alisimamia kikosi cha askari 100.]
6akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.”
7Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.”
8Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.
9Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ naye hufanya.”
10Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii.
11Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni.[#8:11 Luka 13:29. Wokovu wa wakati ujao unaelezwa hapa kwa picha au mfano wa karamu (rejea Isa 25:6; Luka 14:15; Ufu 19:9).]
12Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.”[#8:12 Tafsiri ya neno kwa neno: “watoto wa ufalme” maana yake ni wale ambao ufalme huo ni wao yaani Waisraeli kwa jumla ambao walikuwa kwanza wameahidiwa ufalme huo.; #8:12 Mahali ambamo waovu wataadhibiwa; (taz pia 22:13; 24:51; 25:30).; #8:12 Mfano wa kuelezea ghadhabu na chuki vitakavyowakumba waovu. Msemo huo unatumika pia katika Mat 13:42,50; 22:13; 24:51; 25:30; Luka 13:28.]
13Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile.
14Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali.
15Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia.
16Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa.[#8:16 Neno hili linatumika kutafsiria majina mawili katika Kigiriki yanayowataja viumbe wa kiroho wabaya: “daimonion” na “pneuma akatartha”. Majina mengine yanayotumika katika A.J. kwa viumbe kama hao ni “Shetani” (Kigiriki “satanas”) na “Ibilisi” (Kigiriki “diabolos”). Katika A.J. Ibilisi na Shetani huenda ni majina ya kiumbe yuleyule ambaye ndiye kiongozi wa pepo wabaya.]
17Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie:
“Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu,
ameyabeba magonjwa yetu.”
18Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ng'ambo ya ziwa.[#8:18 Yaani ziwa la Galilaya.]
19Mwalimu mmoja wa sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote utakakokwenda.”[#8:19 Mwandishi wa Injili ya Mathayo anamtaja kuwa mwalimu … wa sheria lakini Luka anamtaja kuwa ni mtu mmoja. Katika taifa la Israeli kulikuweko kundi la waalimu wa sheria ambao walikuwa wataalamu wa sheria na wengi wao walimpinga Yesu na mafundisho yake (taz pia Marko 2:16; Mat 23; 26:57); waliwapinga pia wafuasi wake (Mate 4:5; 6:12).]
20Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.”[#8:20 Katika A.J. isipokuwa tu Mate 7:56 (Stefano ndiye anayeongea hapa), na Ufu 1:13, jina Mwana wa Mtu analitumia Yesu kujitaja yeye mwenyewe. Taz pia Orodha ya Maneno.]
21Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.”
22Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.”[#8:22 Msemo huu ambao ni kama methali una lengo la kuonesha kwamba kumfuata Yesu ni wajibu mkuu kuliko wajibu wa jamaa na jamii. Rejea Mat 10:37; Luka 14:26.]
23Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye.
24Mara, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu lakini alikuwa amelala usingizi.
25Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!”
26Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa.
27Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na bahari vinamtii!”
28Yesu alifika katika nchi ya Wagadara, ng'ambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita njia hiyo.[#8:28 Mahali ambapo waliishi watu wasio Wayahudi. Hati nyingine za kale zina “Gergesa”, na nyingine zina “Gerasa” (Marko 5:1).]
29Nao wakaanza kupiga kelele, “Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?”[#8:29 Hili ni swali ambalo linaonesha hali ya hofu na uadui.]
30Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa.
31Basi, hao pepo wakamsihi, “Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale.”
32Yesu akawaambia, “Haya, nendeni.” Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa majini.
33Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa.
34Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.