Filemoni 1

Filemoni 1

1Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu,[#1 Rejea aya ya 9, na taz Efe 3:1 maelezo.; #1 Taz 2Kor 1:1 maelezo.]

2na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo.[#2 Taz maelezo ya Rom 16:5.; #2 Wengine wanadhani huyu ni mkewe Filemoni.; #2 Yamkini huyu alikuwa mwanawe Filemoni na Afia. Katika Kol 4:17 Arkipo alikuwa na wadhifa fulani katika Kanisa la Kolosai (au katika Kanisa la jirani la Laodikea). Bila shaka Filemoni aliitoa nyumba yake iwe mahali ambapo Kanisa (yaani jumuiya ya Wakristo) lilikutana (taz Rom 16:5 maelezo; rejea Kol 4:15).]

3Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.

Upendo na imani ya Filemoni

4Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu,

5maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu.

6Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo.

7Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.

Ombi kwa ajili ya Onesimo

8Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya.

9Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.

10Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.[#10 Kol 4:9. Katika aya 18 huenda Onesimo alikuwa amechukua fedha au mali ya bwana wake.; #10 1Kor 4:15; Gal 4:19. Paulo anamchukua Onesimo kama mtoto wake kwa sababu Onesimo aliongokea imani ya Kikristo kwa kuongozwa naye mwenyewe.]

11Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.[#11 Maneno yanayotokana na jina lenyewe Onesimo: Kigiriki ni kitenzi chenye maana ya “-a kufaa”, au “-a faida”. Paulo anamwona Onesimo kwamba anafaa kwa kuwa sasa amekuwa mfuasi wa Yesu Kristo na anaweza kumsaidia Paulo kuhubiri Injili (aya 13). “Onesimo” lilikuwa jina la kawaida miongoni mwa watumwa.]

12Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.

13Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili.[#13-14 Onesimo alimtumikia Paulo kifungoni na kwa sababu hiyo Paulo angalipendelea kumweka akae naye; yawezekana kwamba Paulo alitarajia kwamba Filemoni angeweza kumrudisha Onesimo kwake.]

14Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.

15Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima.

16Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.

17Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.

18Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.[#18-19 Paulo anataja uwezekano kwamba Onesimo alipotoroka labda alichukua chochote cha bwana wake naye Paulo anaahidi kwamba atalipa. Lakini, papo hapo, anamkumbusha Filemoni kwamba ana deni lake la kiroho; yamkini yahusu kuongoka kwake Filemoni na kupata uhai mpya kwa njia ya mahubiri ya Paulo.]

19Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako).[#19 Taz 1Kor 16:21.]

20Naam, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.

21Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.[#21 Haisemwi popote kwamba Paulo alimwomba Filemoni amwache huru huyo mtumwa wake. Paulo anamwachia Filemoni hiari yake.]

22Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.[#22 Paulo ana matumaini kwamba atafunguliwa kifungoni na kuweza kwenda Kolosai kumsalimu Filemoni.]

Salamu za mwisho

23Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu.[#23-24 Watu hao hao wanaopeleka salamu zao kwa Filemoni wanatajwa pia katika Kol 4:10-14.]

24Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.

25Nawatakieni nyinyi nyote neema ya Bwana Yesu Kristo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania