The chat will start when you send the first message.
1Je, maisha yenu katika Kristo yanawapeni nguvu? Je, upendo wake unawafarijini? Je, mnao umoja na Roho Mtakatifu na kuoneana huruma na kusikitikiana nyinyi kwa nyinyi?[#2:1 Aya hii ina sentensi tatu ambazo zinatanguliwa na “Je” na katika lugha ya awali inaonekana kwamba zote ni maswali. Lakini ukweli ni kwamba si maswali yanayotaka majibu ila ni mtindo wa kueleza kwa undani kabisa hali ya maisha ya hao Wakristo.]
2Basi, ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na fikira moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja.
3Msifanye chochote kwa moyo wa fitina au kwa majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu nyinyi kwa nyinyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe.[#2:3 Aya hii yamkini yaonesha kwamba hata katika kanisa la huko Filipi kulikuwa na kuoneana wivu, kiasi cha Paulo kuwaonya kusiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe (aya ya 4).]
4Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake.[#2:1-4 Paulo anazungumzia na kutaja kwa undani kiini cha maisha ya Kikristo, yaani kitendo cha wokovu cha Kristo na nafasi ya Roho Mtakatifu.]
5Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu:[#2:5 Au, “Namna ile ile ya kufikiria”. Aya hii inatumika pia kuunganisha aya 1-4 na utenzi unaofuata yaani aya 6-11 na ni kama utangulizi wake.; #2:5-11 Ili kuwapatia Wafilipi msingi ulio imara zaidi kuhusu yote aliyoyasema katika aya zilizotangulia (2-4) Paulo anaingiza hapa mwenendo na tabia yake Kristo mwenyewe. Aya 6-11 zimeandikwa kishairi na zinaeleza kwa ufasaha mkubwa unyenyekevu wa Yesu na kutukuzwa kwake. Wengi wanafikiri utenzi huu ulikuwa sehemu ya ibada ya Kikristo. Tenzi au nyimbo nyingine za namna hii ni: Yoh 1:1-18; Kol 1:15-20; 1Tim 3:16 na Ebr 1:1-14.]
6Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu;[#2:6 Yahusu kuweko kwake Kristo kabla ya kuumbwa ulimwengu (Yoh 1:1-2; 17:5; taz pia Kol 1:15-20).]
lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.
7Bali, kwa hiari yake mwenyewe,
aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi,
akawa sawa na wanadamu,
akaonekana kama wanadamu.
8Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa,[#2:8 Rejea Isa 53:3-9; Mate 8:32-33. Aya ya 6 mpaka 8 zinasema juu ya Yesu kujishusha, hata mpaka kifo cha aibu kuliko vyote. Na kuhusu kutii kwake rejea Isa 53:12; Mat 26:39; Rom 5:19; Ebr 5:8.]
hata kufa msalabani.
9Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa,
akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.
10Ili kwa heshima ya jina la Yesu,
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,
vipige magoti mbele yake,
11na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana,[#2:11 Jina hili la sifa, licha ya kwamba linatumiwa kuhusu watu wenye vyeo, katika Kiswahili cha kawaida linamtaja mwanamume. Lakini katika Biblia linatumika pia kumtaja Mungu hasa katika LXX na katika A.J. Wakristo wa kwanza walilitumia jina hilo kuungama kwamba Kristo alikuwa Mungu (taz 1Kor 12:3 maelezo). Wakati huohuo, katika utenzi huu, “Bwana” ni kinyume cha mtumishi (mtumwa) aya ya 7, na hivyo linatumika kutilia mkazo tofauti iliyopo kati ya kujinyenyekeza na kukwezwa kwake Kristo.]
kwa utukufu wa Mungu Baba.
12Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu,
13kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.
14Fanyeni kila kitu bila kunung'unika na bila ubishi,
15ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtang'ara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga,
16mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure.
17Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo.[#2:17 Rom 12:1; 15:16; 2Tim 4:6. Paulo akijisikia katika mazingira alimo sasa (yaani, ya kifungoni na uwezekano wa kuhukumiwa kifo) anaona uhai wake kuwa si kitu kama utatolewa kwa lengo la kuimarisha imani ya Wafilipi na hivyo kwa ajili ya Injili.]
18Hali kadhalika nanyi mnapaswa kufurahi na kunishirikisha mimi furaha yenu.
19Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu.
20Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo.
21Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo.
22Nyinyi wenyewe mwafahamu jinsi Timotheo alivyo thabiti; yeye na mimi, kama vile mtoto na baba yake, tumefanya kazi pamoja kwa ajili ya Injili.
23Kwa hiyo natumaini kumtuma kwenu mara nitakapojua jinsi mambo yatakavyoniendea.
24Na, ninatumaini katika Bwana kwamba nami pia nitaweza kuja kwenu karibuni.
25Nimeona sina budi kumtuma kwenu ndugu yetu Epafrodito, ambaye ni mwenzangu kazini na vitani na ambaye ni mjumbe wenu aliyenisaidia katika mahitaji yangu.
26Anayo hamu kubwa ya kuwaoneni nyinyi nyote, na amesikitika sana kwani nyinyi mmepata habari kwamba alikuwa mgonjwa.
27Naam, alikuwa mgonjwa hata karibu ya kufa. Lakini Mungu alimwonea huruma, na si yeye peke yake, ila na mimi pia ili nisipate uchungu zaidi.
28Basi, nataka sana kumtuma kwenu, ili mtakapomwona mpate kufurahi tena, nayo huzuni yangu itoweke.
29Mpokeeni, basi, kwa furaha yote kama ndugu katika Bwana. Mnapaswa kuwastahi watu walio kama yeye,
30kwani yeye alikuwa hata karibu ya kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, na kuhatarisha maisha yake ili aweze kunipa mimi msaada ule ambao hamkuweza kuuleta nyinyi wenyewe.