Mhubiri 4

Mhubiri 4

Uonevu, taabu, uadui

1Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua:

Nikaona machozi ya waliodhulumiwa,

wala hawana mfariji;

uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowadhulumu,

lakini hawakuwa na mfariji.

2Nami nikasema kwamba wafu,

waliokwisha kufa,

wana furaha kuliko watu walio hai,

ambao bado wanaishi.

3Lakini aliye bora kuliko hao wawili

ni yule ambaye hajazaliwa bado,

ambaye hajaona ule uovu

unaofanyika chini ya jua.

4Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

5Mpumbavu hukunja mikono yake

na kujiangamiza mwenyewe.

6Afadhali konzi moja pamoja

na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu

na kukimbiza upepo.

7Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:

8Kulikuwa na mtu aliye peke yake,

hakuwa na mwana wala ndugu.

Hapakuwa na mwisho wa kazi yake;

hata hivyo macho yake

hayakutosheka na utajiri wake.

Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,

nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”

Hili pia ni ubatili,

ni shughuli yenye taabu!

9Wawili ni afadhali kuliko mmoja,

kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:

10Kama mmoja akianguka,

mwenzake atamwinua.

Lakini ni jambo la kuhuzunisha

kwa mtu yule aangukaye

naye hana wa kumwinua!

11Pia, kama wawili wakilala pamoja

watapashana joto.

Lakini ni vipi mtu aweza

kujipasha joto mwenyewe?

12Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,

watu wawili wanaweza

kumkabili adui na kumshinda.

Kamba ya nyuzi tatu

haikatiki kwa urahisi.

Maendeleo ni ubatili

13Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo.

14Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme.

15Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme.

16Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.