Kutoka 35

Kutoka 35

Masharti ya Sabato

1Musa akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndio mambo ambayo Bwana amewaamuru ninyi mfanye:

2Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya mapumziko kwa Bwana . Yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe.

3Msiwashe moto mahali popote katika makazi yenu siku ya Sabato.”

Vifaa kwa ajili ya maskani ya Mungu

(Kut 25:1‑9)

4Musa akaiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo Bwana aliloamuru:

5Toeni sadaka kwa Bwana kutoka mali mliyo nayo. Kila mmoja aliye na moyo wa kupenda atamletea Bwana sadaka ya:

“dhahabu, fedha na shaba;

6nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi;

singa za mbuzi;

7ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo;[#35:7 pengine ni mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili]

mbao za mshita;

8mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa;

vikolezo kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri;

9vito vya shohamu, na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kizibau na kile kifuko cha kifuani.

10“Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kitu Bwana alichoamuru:

11“Maskani ya Mungu pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako;

12Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia;

13meza na mipiko yake, pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonesho;

14kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga;

15madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri;

pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya Maskani;

16madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote;

sinia la shaba pamoja na tako lake;

17pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, na pazia la ingilio la ua;

18vigingi vya hema kwa ajili ya Maskani pamoja na ua na kamba zake;

19mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Haruni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.”

20Ndipo jumuiya yote ya Waisraeli ilipoondoka mbele ya Musa,

21na kila mmoja aliyependa na ambaye moyo wake ulimsukuma alikuja na kuleta sadaka kwa Bwana , kwa ajili ya kazi katika Hema la Kukutania, kwa ajili ya huduma yake yote na kwa ajili ya mavazi matakatifu.

22Wote waliopenda, wanaume na wanawake, wakaja wakaleta vito vya dhahabu vya kila aina: vipini, vipuli, pete na mapambo. Wote wakatoa dhahabu zao kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana .

23Kila mmoja aliyekuwa na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi, au singa za mbuzi, ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, au ngozi za pomboo, wakavileta.

24Wale waliotoa sadaka ya fedha au shaba wakavileta kama sadaka kwa Bwana , na kila aliyekuwa na mti wa mshita kwa ajili ya kazi yoyote ile akauleta.

25Kila mwanamke aliyekuwa na ujuzi alisokota kwa mikono yake na alileta kile alichosokota, iwe ni nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi.

26Wanawake wote waliopenda na waliokuwa na ujuzi wakasokota singa za mbuzi.

27Viongozi wakaleta vito vya shohamu pamoja na vito vingine vya thamani kwa ajili ya kuweka kwenye kizibau na kwenye kifuko cha kifuani.

28Wakaleta pia vikolezo na mafuta ya zeituni kwa ajili ya mwanga, kwa ajili ya mafuta ya upako na kwa ajili ya uvumba wenye harufu nzuri.

29Waisraeli wote, wanaume na wanawake, waliopenda wakaleta mbele za Bwana kwa hiari yao wenyewe sadaka kwa ajili ya kazi yote ya Bwana aliyokuwa amewaagiza kuifanya kupitia kwa Musa.

Bezaleli na Oholiabu

(Kut 31:1‑11)

30Kisha Musa akawaambia Waisraeli, “Tazameni, Bwana amemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda,

31naye amemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, na uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi,

32ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba,

33kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi wa kupendeza.

34Tena amempa yeye pamoja na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, uwezo wa kufundisha wengine.

35Amewajaza ustadi wa kufanya kazi za aina zote zinazofanywa na mafundi, na wenye kubuni michoro, pia na watarizi kwa rangi za buluu, zambarau, nyekundu na kitani safi, na wafumaji: wote wakiwa mafundi na wabunifu hodari.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.