The chat will start when you send the first message.
1Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa.
2Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia?
3Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili?
4Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure!
5Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza kati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?
6Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”[#3:6 Mwa 15:6]
7Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu.
8Andiko liliona tangu awali kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, hivyo likatangulia kumtangazia Abrahamu Injili, likisema kwamba, “Kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.”[#3:8 Mwa 12:3; 18:18; 22:18]
9Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.
10Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.”[#3:10 Kum 27:26]
11Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”[#3:11 Hab 2:4]
12Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”[#3:12 Law 18:5]
13Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.”[#3:13 Kum 21:23]
14Alitukomboa ili baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kupitia kwa Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.
15Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii.
16Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa uzao”, yakimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako”, yaani mtu mmoja, ndiye Kristo.[#3:16 Mwa 12:7; 13:15; 24:7]
17Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka mia nne na thelathini (430) baadaye, haitangui agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile.
18Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kupitia kwa ahadi.
19Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa hadi atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.
20Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.
21Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kupitia kwa sheria.
22Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kupitia kwa imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.
23Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa hadi ile imani ifunuliwe.
24Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani.
25Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.
26Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kupitia kwa imani.
27Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo.
28Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu.
29Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.