Hosea 1

Hosea 1

1Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli.

Mke wa Hosea na watoto wake

2Bwana alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, Bwana alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha Bwana .”

3Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana.

4Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite jina Yezreeli, kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli.[#1:4 maana yake Mungu hupanda]

5Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.”

6Gomeri akachukua tena mimba akamzaa binti. Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Lo-Ruhama, kwa maana sitaonesha tena upendo kwa nyumba ya Israeli, kwamba nisije kabisa nikawasamehe.[#1:6 maana yake Sio mpendwa wangu]

7Hata hivyo nitaonesha upendo kwa nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa si kwa upinde, upanga au vita, wala kwa farasi na wapanda farasi, bali kupitia Bwana Mungu wao.”

8Baada ya Gomeri kumwachisha Lo-Ruhama kunyonya, Gomeri alipata mwana mwingine.

9Kisha Bwana akasema, “Mwite Lo-Ami kwa maana ninyi si watu wangu, nami si Mungu wenu.[#1:9 maana yake Sio watu wangu]

10“Hata hivyo Waisraeli watakuwa kama mchanga kando ya bahari, ambao hauwezi kupimika wala kuhesabiwa. Mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai’.

11Watu wa Yuda na watu wa Israeli wataunganishwa tena, nao watamchagua kiongozi mmoja nao watakwea watoke katika nchi, kwa kuwa siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.