Isaya 10

Isaya 10

1Ole wao wawekao sheria zisizo za haki,

kwa wale watoao amri za kuonea,

2kuwanyima maskini haki zao

na kuzuilia haki za watu wangu waliodhulumiwa,

kuwafanya wajane mawindo yao

na kuwanyangʼanya yatima.

3Mtafanya nini siku ya hukumu,

wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali?

Mtamkimbilia nani awape msaada?

Mtaacha wapi mali yenu?

4Hakutasalia kitu chochote,

isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka,

au kuanguka miongoni mwa waliouawa.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

Hukumu ya Mungu juu ya Ashuru

5“Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu,

ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu!

6Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu,

ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha,

kukamata mateka na kunyakua nyara,

pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani.

7Lakini hili silo analokusudia,

hili silo alilo nalo akilini;

kusudi lake ni kuangamiza,

kuyakomesha mataifa mengi.

8Maana asema, ‘Je, wafalme wote

si majemadari wangu?

9Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi?

Hamathi si kama Arpadi,

nayo Samaria si kama Dameski?

10Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu,

falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:

11je, nisiutendee Yerusalemu na sanamu zake

kama nilivyoutendea Samaria na vinyago vyake?’ ”

12Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.”

13Kwa kuwa anasema:

“ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili,

kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu.

Niliondoa mipaka ya mataifa,

niliteka nyara hazina zao,

kama yeye aliye shujaa

niliwatiisha wafalme wao.

14Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota,

ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa;

kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa,

ndivyo nilivyokusanya nchi zote;

wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa

au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”

15Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu

kuliko yule anayelitumia,

au msumeno kujisifu

dhidi ya yule anayeutumia?

Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye,

au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!

16Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi,

atatuma ugonjwa wa kudhoofisha

kwa mashujaa wake wanene,

katika fahari yake moto utawaka

kama mwali wa moto.

17Nuru ya Israeli itakuwa moto,

Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto;

katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba

na michongoma yake.

18Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba

utateketeza kabisa,

kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.

19Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana

hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu.

Mabaki ya Israeli

20Katika siku ile, mabaki ya Israeli,

walionusurika wa nyumba ya Yakobo,

hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga,

lakini watamtegemea kwa kweli

Bwana Aliye Mtakatifu wa Israeli.

21Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo[#10:21 Kiebrania ni Shear-Yashubu ; pia 10:22.]

watamrudia Mungu Mwenye Nguvu.

22Ingawa watu wako, ee Israeli,

ni wengi kama mchanga wa pwani,

ni mabaki yao tu watakaorudi.

Maangamizi yamekwisha amriwa,

ni mengi tena ni haki.

23Bwana, Bwana wa majeshi, atatekeleza

maangamizi yaliyoamriwa juu ya nchi yote.

24Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana, Bwana wa majeshi:

“Enyi watu wangu mnaoishi Sayuni,

msiwaogope Waashuru,

wanaowapiga ninyi kwa fimbo

na kuinua rungu dhidi yenu, kama Misri ilivyofanya.

25Bado kitambo kidogo sana hasira yangu dhidi yenu itakoma,

na ghadhabu yangu itaelekezwa kwenye maangamizi yao.”

26Bwana wa majeshi atawachapa kwa mjeledi,

kama alivyowapiga Wamidiani katika mwamba wa Orebu,

naye atainua fimbo yake juu ya maji,

kama alivyofanya huko Misri.

27Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa kutoka mabegani mwenu,

na nira yao kutoka shingoni mwenu;

nira itavunjwa

kwa sababu ya kupakwa mafuta.

28Wanaingia Ayathi,

wanapita katikati ya Migroni,

wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi.

29Wanavuka kivukoni, nao wanasema,

“Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.”

Rama inatetemeka;

Gibea ya Sauli inakimbia.

30Piga kelele, ee Binti Galimu!

Sikiliza, ee Laisha!

Maskini Anathothi!

31Madmena inakimbia;

watu wa Gebimu wanajificha.

32Siku hii ya leo watasimama Nobu;

watatikisa ngumi zao

kwa mlima wa Binti Sayuni,

kwa kilima cha Yerusalemu.

33Tazama, Bwana, Bwana wa majeshi,

atayakata matawi kwa nguvu kuu.

Miti mirefu sana itaangushwa,

ile mirefu itashushwa chini.

34Atakata vichaka vya msitu kwa shoka;

Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.