Waamuzi 14

Waamuzi 14

Ndoa ya Samsoni

1Samsoni akateremka Timna, na huko akamwona mwanamke Mfilisti.

2Alipopanda kutoka huko, akawaambia baba yake na mama yake, “Nimemwona mwanamke Mfilisti huko Timna; basi mnitwalie awe mke wangu.”

3Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa watu wetu wote, hata ulazimike kwenda kujitwalia mke kutoka kwa hao Wafilisti wasiotahiriwa?”

Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye alinipendeza.”

4(Baba yake na mama yake hawakujua kuwa jambo hili limetoka kwa Bwana , kwani alikuwa akitafuta sababu ya kukabiliana na Wafilisti; kwa kuwa wakati huo walikuwa wakiwatawala Waisraeli.)

5Samsoni akateremka Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia.

6Roho wa Bwana akaja juu ya Samsoni kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono mitupu kama ambavyo angempasua mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake alichokifanya.

7Basi akateremka na kuongea na yule mwanamke, naye akampendeza Samsoni.

8Baada ya muda, Samsoni aliporudi ili akamwoe, akageuka kando ili kuutazama mzoga wa yule simba. Tazama! Ndani ya ule mzoga akaona kundi la nyuki na asali kiasi.

9Akachukua asali mkononi mwake, akala huku akitembea. Alipowafikia baba yake na mama yake, akawapa kiasi cha ile asali, nao wakala. Lakini hakuwaambia kuwa aliitwaa asali katika mzoga wa simba.

10Basi baba yake akateremka kumwona huyo mwanamke. Samsoni akafanya karamu huko, kama ilivyokuwa desturi ya vijana.

11Watu walipomwona, wakaleta vijana wenzake thelathini ili kuwa pamoja naye.

12Samsoni akawaambia, “Niwape kitendawili, mkiweza kunipa jibu katika muda wa siku hizi saba za karamu, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.

13Lakini msipoweza kufumbua, ndipo ninyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.”

Wakamwambia, “Tuambie hicho kitendawili, hebu na tukisikie.”

14Akawaambia,

“Ndani ya mlaji,

kulitoka kitu cha kuliwa,

ndani ya mwenye nguvu,

kulitoka kitu kitamu.”

Kwa muda wa siku tatu hawakuweza kutoa jibu.

15Siku ya nne, wakamwambia mkewe Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atutegulie hicho kitendawili, la sivyo tutakuchoma moto wewe na wa nyumba ya baba yako. Je, mmetualika ili mpate kutunyangʼanya kile tulicho nacho?”

16Basi mke wa Samsoni akalia mbele yake na kumwambia, “Unanichukia! Hunipendi kabisa. Umewategea watu wangu kitendawili, lakini mimi hujaniambia jibu.”

Samsoni akamwambia, “Tazama, sijamweleza baba yangu wala mama yangu, kwa nini nikufumbulie?”

17Mkewe akalia kwa muda wa zile siku zote saba za karamu. Hivyo siku ya saba Samsoni akamweleza, kwa kuwa aliendelea kumsisitiza sana. Naye mkewe akawaeleza watu wake kile kitendawili.

18Siku ya saba, kabla ya jua kutua, wanaume wa mji wakamwambia Samsoni,

“Ni nini kilicho kitamu kuliko asali?

Ni nini chenye nguvu kuliko simba?”

Samsoni akawaambia,

“Kama hamkulima na mtamba wangu,

msingekitegua kitendawili changu.”

19Ndipo Roho wa Bwana akamjia Samsoni kwa nguvu. Samsoni akateremka hadi Ashkeloni, akawaua wanaume thelathini wa mji huo, akatwaa mali yao, akawapa watu wale waliotegua kile kitendawili nguo zao. Akiwa amejaa hasira, akakwea kurudi nyumbani kwa baba yake.

20Naye mke wa Samsoni akakabidhiwa kwa rafiki yake Samsoni aliyekuwa msaidizi wake siku ya arusi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.