The chat will start when you send the first message.
1Baada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni pa Bwana .
2Hivyo Bwana akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi huko Haroshethi-Hagoyimu.[#4:2 yaani Haroshethi ya Mataifa]
3Kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya vita ya chuma yapatayo mia tisa, naye alikuwa amewatesa Waisraeli kwa ukatili kwa muda wa miaka ishirini, Waisraeli wakamlilia Bwana wakaomba msaada.
4Debora, nabii mwanamke, mkewe Lapidothi, ndiye alikuwa anaamua Israeli wakati ule.
5Debora alikuwa akiketi chini ya Mtende wa Debora uliokuwa kati ya Rama na Betheli katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakaja kwake ili awaamue.
6Akatuma wamwite Baraka mwana wa Abinoamu kutoka Kedeshi huko Naftali na kumwambia, “Bwana , Mungu wa Israeli, anakuagiza: ‘Nenda, chukua wanaume elfu kumi toka Naftali na Zabuloni, mwende Mlima Tabori.
7Nitamshawishi Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, pamoja na magari yake ya vita na jeshi lake, hadi Mto Kishoni na kumtia mikononi mwako.’ ”
8Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami nitaenda, lakini usipoenda pamoja nami, sitaenda.”
9Debora akamwambia, “Hakika nitaenda pamoja nawe, lakini njia unayoiendea haitakupa heshima wewe, kwa kuwa Bwana atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Hivyo Debora akaenda pamoja na Baraka hadi Kedeshi,
10ambapo Baraka aliwaita Zabuloni na Naftali. Watu elfu kumi wakamfuata Baraka, na Debora pia akaenda naye.
11Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wale wengine, yaani wazao wa Hobabu, mkwewe Musa, naye akapiga hema lake karibu na ule mti mkubwa wa mwaloni ulio Saananimu, karibu na Kedeshi.
12Sisera alipoambiwa kuwa Baraka mwana wa Abinoamu alikuwa amepanda Mlima Tabori,
13Sisera akakusanya magari yake ya vita ya chuma mia tisa, na watu wote waliokuwa pamoja naye, kuanzia Haroshethi-Hagoyimu hadi Mto wa Kishoni.
14Ndipo Debora akamwambia Baraka, “Nenda! Hii ndiyo siku ambayo Bwana amemtia Sisera mikononi mwako. Je, Bwana hakukutangulia mbele yako?” Hivyo Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori, akifuatwa na watu elfu kumi.
15Bwana akamfadhaisha Sisera na magari yake ya vita yote, pamoja na jeshi lake lote kwa upanga mbele ya Baraka, naye Sisera akaliacha gari lake la vita na kukimbia kwa miguu.
16Lakini Baraka akafuata magari ya vita pamoja na jeshi hadi Haroshethi-Hagoyimu. Jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga, wala hakuna hata mtu mmoja aliyesalia.
17Sisera, hata hivyo, akakimbia kwa miguu hadi kwenye hema la Yaeli, mkewe Heberi, Mkeni, kwa sababu palikuwa na uhusiano wa kirafiki kati ya Yabini mfalme wa Hazori na ukoo wa Heberi, Mkeni.
18Yaeli akaenda kumlaki Sisera na kumwambia, “Karibu, bwana wangu, karibu ingia ndani kabisa. Usiogope.” Basi Sisera akaingia ndani ya hema la Yaeli, naye akamfunika kwa blanketi nene.
19Akamwambia, “Nina kiu, tafadhali nipe maji ya kunywa.” Ndipo akafungua kiriba cha maziwa na kumpa akanywa, kisha akamfunika.
20Naye Sisera akamwambia, “Simama mlangoni pa hema na mtu yeyote akija na kukuuliza, ‘Je, kuna mtu yeyote hapa?’ sema, ‘Hapana.’ ”
21Lakini Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akachukua nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akiwa amelala usingizi kwa kuchoka. Akakipigilia kile kigingi kwenye paji la uso wake, kikapenya hata kuingia ardhini, naye akafa.
22Baraka akakaribia akimfuatia Sisera, Yaeli akatoka kumlaki. Akamwambia, “Njoo, nitakuonesha mtu unayemtafuta.” Hivyo wakaingia ndani ya hema, na tazama, Sisera alikuwa amelala humo akiwa amekufa, na hicho kigingi cha hema kikiwa kimepigiliwa kupitia paji la uso wake.
23Basi siku ile Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani, mbele ya Israeli.
24Nao mkono wa Waisraeli ukaendelea kuwa na nguvu zaidi na zaidi dhidi ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hadi wakamwangamiza.