The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:
2“Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa?
Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?
3Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya?
Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?
4Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili
nami ni safi mbele zako.’
5Aha! Laiti kwamba Mungu angesema,
kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,
6naye akufunulie siri za hekima,
kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili.
Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.
7“Je, unaweza kujua siri za Mungu?
Je, unaweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?
8Ni juu mno kuliko mbingu: unaweza kufanya nini?
Kina chake ni kirefu kuliko Kuzimu:
wewe unaweza kujua nini?
9Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia,
nacho ni kipana kuliko bahari.
10“Akija na kukufunga gerezani,
na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?
11Hakika anawatambua watu wadanganyifu;
naye aonapo uovu, je, haangalii?
12Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima,
endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.
13“Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake
na kumwinulia mikono yako,
14ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako,
wala usiuruhusu uovu ukae kwenye hema lako,
15ndipo utainua uso wako bila aibu;
utasimama imara bila hofu.
16Hakika utaisahau taabu yako,
utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.
17Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri,
nalo giza litakuwa kama alfajiri.
18Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini;
utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.
19Utalala, wala hakuna atakayekuogofya,
naam, wengi watajipendekeza kwako.
20Bali macho ya waovu hayataona,
wokovu utawaepuka;
tarajio lao litakuwa ni hangaiko
la mtu anayekata roho.”