Mika 2

Mika 2

Mipango ya mwanadamu na mipango ya Mungu

1Ole kwa wale wapangao uovu,

kwa wale wapangao hila vitandani mwao!

Kunapopambazuka wanalitimiza

kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.

2Wanatamani mashamba na kuyakamata,

pia nyumba na kuzichukua.

Wanamlaghai mwanaume nyumba yake,

mwanadamu mwenzake urithi wake.

3Kwa hiyo, Bwana asema:

“Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa,

ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe.

Hamtatembea tena kwa majivuno,

kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa.

4Siku hiyo watu watawadhihaki,

watawafanyia mzaha

kwa wimbo huu wa maombolezo:

‘Tumeangamizwa kabisa;

mali ya watu wangu imegawanywa.

Ameninyangʼanya!

Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ”

5Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la Bwana

wa kugawanya mashamba kwa kura.

Manabii wa uongo

6Manabii wao husema, “Usitabiri.

Usitabiri kuhusu vitu hivi;

aibu haitatupata.”

7Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo:

“Je, Roho wa Bwana amekasirika?

Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?”

“Je, maneno yangu hayamfanyii mema

yeye ambaye njia zake ni nyofu?

8Siku hizi watu wangu wameinuka

kama adui.

Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita

pasipo kujali,

kama watu warudio kutoka vitani.

9Unawahamisha wanawake wa watu wangu

kutoka nyumba zao za kupendeza.

Unaondoa baraka yangu

kwa watoto wao milele.

10Inuka, nenda zako!

Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia,

kwa sababu pametiwa unajisi,

pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena.

11Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema,

‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’

angekuwa ndiye nabii

anayekubalika na watu hawa!

Ahadi ya ukombozi

12“Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo,

Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli.

Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi,

kama kundi kwenye malisho yake,

mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu.

13Yeye afunguaye njia atawatangulia;

watapita kwenye lango na kutoka nje.

Mfalme wao atawatangulia,

Bwana atakuwa kiongozi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.