Zaburi 37

Zaburi 37

Zaburi 37

Mwisho wa mwovu na urithi wa mwenye haki

1Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,

wala usiwaonee wivu watendao mabaya,

2kwa maana watanyauka upesi kama majani,

watakufa upesi kama mimea ya kijani.

3Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema.

Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

4Jifurahishe katika Bwana

naye atakupa haja za moyo wako.

5Mkabidhi Bwana njia yako,

mtumaini yeye, naye atatenda hili:

6Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko,

na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.

7Tulia mbele za Bwana

na umngojee kwa uvumilivu;

usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,

wanapotekeleza mipango yao miovu.

8Epuka hasira na uache ghadhabu;

usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.

9Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,

bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi.

10Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana,

ingawa utawatafuta, hawataonekana.

11Bali wanyenyekevu watairithi nchi

na wafurahie amani tele.

12Waovu hula njama dhidi ya wenye haki

na kuwasagia meno,

13bali Bwana huwacheka waovu,

kwa sababu anajua siku yao inakuja.

14Waovu hufuta upanga

na kupinda upinde,

ili wawaangushe maskini na wahitaji,

kuwaua wale ambao njia zao ni nyofu.

15Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe,

na pinde zao zitavunjwa.

16Bora kidogo walicho nacho wenye haki

kuliko wingi wa mali ya waovu wengi;

17kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa,

lakini Bwana humtegemeza mwenye haki.

18Bwana anazifahamu siku za wanyofu,

na urithi wao utadumu milele.

19Siku za maafa hawatanyauka,

siku za njaa watafurahia wingi wa vitu.

20Lakini waovu wataangamia:

Adui za Bwana watakuwa

kama uzuri wa mashamba,

watatoweka,

watatoweka kama moshi.

21Waovu hukopa na hawalipi,

bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.

22Wale wanaobarikiwa na Bwana watairithi nchi,

bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.

23Kama Bwana akipendezwa na njia ya mtu,

yeye huimarisha hatua zake,

24ajapojikwaa, hataanguka,

kwa maana Bwana

humtegemeza kwa mkono wake.

25Nilikuwa kijana na sasa ni mzee,

lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa

au watoto wao wakiombaomba chakula.

26Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti.

Watoto wao watabarikiwa.

27Acha ubaya na utende wema,

nawe utaishi katika nchi milele.

28Kwa kuwa Bwana huwapenda wenye haki

naye hatawaacha waaminifu wake.

Watalindwa milele,

lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali.

29Wenye haki watairithi nchi,

na kuishi humo milele.

30Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima,

nao ulimi wake huzungumza lililo haki.

31Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake;

nyayo zake hazitelezi.

32Watu waovu huvizia wenye haki,

wakitafuta kuwaua;

33lakini Bwana hatawaacha mikononi mwao

wala hatawaacha wahukumiwe

kuwa wakosa wanaposhtakiwa.

34Mngojee Bwana ,

na uishike njia yake.

Naye atakutukuza uirithi nchi,

waovu watakapokatiliwa mbali,

utaliona hilo.

35Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi

kama mwerezi wa Lebanoni,

36lakini alitoweka upesi na hakuonekana,

ingawa nilimtafuta, hakupatikana.

37Watafakari watu wasio na hatia,

wachunguze watu wakamilifu,

kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani.

38Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa,

mafanikio yao yatakatiliwa mbali.

39Wokovu wa wenye haki hutoka kwa Bwana ,

yeye ni ngome yao wakati wa shida.

40Bwana huwasaidia na kuwaokoa,

huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi,

kwa maana wanamkimbilia.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.