The chat will start when you send the first message.
1Ni vyema kumshukuru Bwana
na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,
2kuutangaza upendo wako asubuhi,
na uaminifu wako wakati wa usiku,
3kwa zeze yenye nyuzi kumi
na kwa sauti ya kinubi.
4Ee Bwana , kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha,
nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.
5Ee Bwana , tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako,
tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako!
6Mjinga hafahamu,
mpumbavu haelewi,
7ingawa waovu huchipua kama majani
na wote watendao maovu wanastawi,
wataangamizwa milele.
8Bali wewe, Ee Bwana ,
utatukuzwa milele.
9Ee Bwana , hakika adui zako,
hakika adui zako wataangamia.
Wote watendao maovu watatawanyika.
10Umeitukuza pembe yangu kama ile ya nyati dume,[#92:10 pembe inawakilisha nguvu]
mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu.
11Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa,
masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu.
12Wenye haki watastawi kama mtende,
watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni,
13waliopandwa katika nyumba ya Bwana ,
watastawi katika nyua za Mungu wetu.
14Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda,
watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu,
15wakitangaza, “Bwana ni mkamilifu;
yeye ni Mwamba wangu,
na ndani yake hamna uovu.”