The chat will start when you send the first message.
1Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua sheria: Je, hamjui kwamba sheria ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu?
2Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa.
3Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.
4Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia sheria kupitia kwa mwili wa Kristo, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu.
5Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na sheria zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti.
6Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na sheria ili tutumike katika njia mpya ya Roho, wala si katika njia ya zamani ya sheria iliyoandikwa.
7Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini singejua dhambi isipokuwa kwa sababu ya sheria. Singejua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.”[#7:7 Kut 20:17; Kum 5:21]
8Lakini dhambi ilipata nafasi katika amri, nayo ikazaa kila aina ya tamaa ndani yangu. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa.
9Mwanzoni nilikuwa hai pasipo sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa.
10Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti.
11Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua.
12Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.
13Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kupitia kwa amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.
14Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi.
15Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia.
16Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema.
17Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
18Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote linalokaa ndani yangu, yaani katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda.
19Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo.
20Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
21Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo.
22Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu.
23Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.
24Ole wangu, mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25Namshukuru Mungu anayeniokoa kupitia kwa Yesu Kristo Bwana wetu!
Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.