Wimbo 4

Wimbo 4

1Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu!

Ee, jinsi ulivyo mzuri!

Macho yako nyuma ya shela yako

ni kama ya hua.

Nywele zako ni kama kundi la mbuzi

wakishuka kutoka Mlima Gileadi.

2Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi,

wanaotoka kuogeshwa.

Kila jino lina pacha lake;

hakuna hata moja lililo pekee.

3Midomo yako ni kama uzi mwekundu,

kinywa chako kinapendeza.

Mashavu yako nyuma ya shela yako

ni kama vipande viwili vya komamanga.

4Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,

uliojengwa kwa madaha,

juu yake zimetundikwa ngao elfu,

zote ni ngao za mashujaa.

5Matiti yako mawili ni kama wana-paa wawili,

kama wana-paa mapacha

wajilishao kati ya yungiyungi.

6Hata kupambazuke na vivuli vikimbie,

nitaenda kwenye mlima wa manemane

na kwenye kilima cha uvumba.

7Wewe ni mzuri kote, mpendwa wangu,

hakuna hitilafu ndani yako.

8Nenda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu,

nenda nami kutoka Lebanoni.

Shuka kutoka ncha ya Amana,

kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,

kutoka mapango ya simba

na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.

9Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu;

umeiba moyo wangu

kwa mtazamo mmoja wa macho yako,

kwa kito kimoja cha mkufu wako.

10Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,

dada yangu, bibi arusi wangu!

Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai,

na harufu ya marhamu yako zaidi ya manukato yoyote!

11Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,

bibi arusi wangu;

maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.

Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.

12Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,

bibi arusi wangu;

wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa,

chemchemi yangu peke yangu.

13Mimea yako ni bustani ya mikomamanga

yenye matunda mazuri sana,

yenye hina na nardo,

14nardo na zafarani,

mchai na mdalasini,

pamoja na kila aina ya mti wa uvumba,

manemane na udi,

na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.

15Wewe ni chemchemi ya bustani,

kisima cha maji yanayotiririka,

yakitiririka kutoka Lebanoni.

16Amka, upepo wa kaskazini,

na uje, upepo wa kusini!

Vuma juu ya bustani yangu,

ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ngʼambo.

Mpenzi wangu na aje bustanini mwake

na kuonja matunda mazuri sana.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.