1 Wamakabayo 7

1 Wamakabayo 7

Safari ya Bakide na Alkimo

1Katika mwaka wa mia moja na hamsini na moja Demetrio, mwana wa Seleuko, alirudi kutoka Rumi, akaenda pamoja na watu wachache kwenye mji wa pwani akajitawaza huko.

2Ikawa, alipokwenda kwenye jumba la kifalme la baba zake, wakuu wa jeshi waliwashika Antioko na Lisia wakawaleta kwake.

3Alipoambiwa yaliyofanyika alisema, Nisiwaone!

4Askari wakawaua, naye Demetrio aliketi katika kiti cha enzi.

5Nao Waisraeli wote walioasi na kuikana dini yao walimjia, pamoja na Alkimo, kiongozi wao, aliyetaka kuwa kuhani mkuu,

6wakawashtaki watu kwa mfalme, wakisema, Yuda na watu wake wamewaharibu rafiki zako wote, na kututawanya mbali na kwetu.

7Basi, tuma mtu unayemwamini aende akatazame jinsi alivyotuangamiza sisi na nchi ya mfalme; akawaadhibu, pamoja na wote waliowasaidia.

8Mfalme akamchagua Bakide, mmoja wa rafiki za mfalme, kiongozi wa nchi ng'ambo ya mto, mtu mkubwa katika ufalme, tena mwaminifu kwa mfalme.

9Akampeleka pamoja na yule mwovu Alkimo, ambaye alimthibitisha katika kazi ya kuhani mkuu, akimwamuru awapatilize wana wa Israeli.

10Wakaondoka na jeshi kubwa, wakaja katika nchi ya Uyahudi, wakatuma wajumbe kuwadanganya Yuda na ndugu zake kwa maneno ya amani.

11Lakini hawakujali maneno yao, maana waliona wamekuja na jeshi kubwa.

12Jamii ya waandishi waliwaendea Alkimo na Bakide kutaka haki,

13na Wahasidimu walikuwa wa kwanza na wana wa Israeli kuomba amani kwao,

14maana walisema, Kuhani wa ukoo wa Haruni amekuja na askari, naye hatatudhulumu.

15Akawapa maneno ya amani na kuwaapia kwamba, Hatuna maazimio mabaya kwenu wala kwa rafiki zenu.

16Wakamsadiki. Lakini mara alishika watu sitini miongoni mwao akawaua kwa siku moja, kama ilivyoandikwa:

17Waliitupa miili ya watakatifu wako[#Zab 79:2-3]

Na kuimwaga damu yao

Pande zote za Yerusalemu,

Wala hapakuwa na mzishi.

18Watu wote wakatishwa na kuona hofu kwa sababu yao, wakisema, Kwao hakuna kweli wala haki; wamelivunja agano na kiapo walichokiapa!

19Bakide akaondoka Yerusalemu akapiga kambi yake Bezetha. Akatuma watu kukamata watoro wengi waliokuwa kwake na watu wengine, akawaua, akawatupa katika shimo kubwa.

20Akamkabidhi Alkimo utawala wa nchi, akamwachia askari wa kumsaidia, kisha aliondoka akamrudia mfalme.

21Alkimo akaipigania kazi yake ya kuhani mkuu,

22na wenye matata wote wakajiweka upande wake, wakaitiisha nchi ya Uyahudi na kufanya hasara nyingi.

23Yuda akayaona mabaya yote ambayo Alkimo na wenzake wamewafanyia Waisraeli – kupita yale ya mataifa –

24akazunguka kwenye mipaka ya Uyahudi akiwapatiliza wale waliomtoroka, na kuwazuia wasiondoke.

25Alkimo alipoona ya kuwa Yuda na watu wake wamepata nguvu, wala hawezi kushindana nao, alikwenda tena kwa mfalme akawasingizia mabaya.

Nikano katika Yuda

26Mfalme akamtuma Nikano, mmoja wa wakuu wake wastahiki, mtu aliyewachukia Waisraeli na kuwa adui yao, akampa amri kuwaharibu watu hao.

27Nikano akaja Yerusalemu na jeshi kubwa, akawadanganya Yuda na ndugu zake kwa maneno ya amani,

28akisema, Isiwepo vita kati yetu. Nitakuja na watu wachache tu, ili niwatazame nyuso zenu kwa amani.

29Akaingia Uyahudi, wakaamkiana kwa amani, lakini adui walikuwa wamejiweka tayari kumkamata Yuda.

30Jambo hilo lilibainika kwa Yuda, akamwonea hofu, asikubali kumwona tena.

31Nikano alipoona shauri lake limetambulikana, akatoka kupigana na Yuda huko Kafasalama.

32Watu wa Nikano wapatao mia tano wakaanguka, na wengine waliikimbilia ngome ya mji wa Daudi.

Nikano anatishia hekalu

33Baada ya hayo, Nikano alipanda kwenda mlima Sayuni, na makuhani wengine wakatoka katika patakatifu, pamoja na wazee wengine, ili kumsalimu kwa amani na kumwonesha sadaka ya kuteketezwa iliyokuwa ikitolewa kwa kumwombea mfalme.

34Bali aliwadhihaki na kuwafanyia mzaha, akawaaibisha na kutoa maneno ya dharau.

35Akaapa kwa hasira, Kama Yuda na jeshi lake hawatiwi mikononi mwangu, itakuwa, nitakaporudi kwa amani, nitaiteketeza kabisa nyumba hii. Akaondoka kwa hasira nyingi.

36Makuhani wakaingia, wakasimama mbele ya madhabahu na patakatifu wakilia.

37Wakasema, Wewe uliyeichagua nyumba hii iitwe kwa jina lako, iwe nyumba ya sala na dua kwa watu wako,

38uwapatilize mtu huyu na jeshi lake, waanguke kwa upanga. Uzikumbuke kufuru zao, uyafute makao yao.

Kifo cha Nikano

39Nikano akaondoka Yerusalemu akapiga kambi Beth-horoni, na jeshi la Shamu likakutana naye pale.

40Yuda naye alipiga kambi yake Adasa na watu elfu tatu.

41Yuda akasali akisema, Watu wa mfalme walipotukana, malaika wako akatoka akapiga watu elfu mia moja na themanini na tano miongoni mwao.[#2 Fal 19:35]

42Basi, vivi hivi ulipige jeshi hili mbele yetu leo, ili wale watakaosalia wajue ya kuwa ametukana patakatifu pako. Umhukumu sawasawa na uovu wake.

43Majeshi yakapambana vitani siku ya kumi na tatu ya mwezi Adari, jeshi la Nikano likashindwa. Yeye mwenyewe alianguka katika mapigano ya kwanza,

44hata askari wake walipoona ya kuwa ameanguka walitupa silaha zao wakakimbia.

45Wakawafuatia mwendo wa kutwa kutoka Adasa hata kufika Gazara; wakapiga tarumbeta za ishara.

46Watu wakatoka katika miji yote ya Uyahudi iliyozunguka, wakaanza kuwazunguka pande zote; wakawarudisha nyuma,

47hata wote wakaanguka kwa upanga, asibaki hata mmoja. Wakachukua nyara na mateka, wakamkata Nikano kichwa na ule mkono wa kuume aliounyosha kwa ufidhuli, wakavileta na kuvitungika Yerusalemu.

48Watu wakafurahi sana, wakiadhimisha siku ile kwa shangwe kuu.

49Wakaagiza iadhimishwe kila mwaka, siku ya kumi na tatu ya Adari.

50Nchi ya Uyahudi ikatulia kitambo.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania