The chat will start when you send the first message.
1Kisha Ayubu akaendelea na hoja yake, na kusema,
2Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu;[#Ayu 34:5]
Huyo Mwenyezi aliyeitesa nafsi yangu;
3(Kwa kuwa uhai wangu ungali mzima ndani yangu,
Na Roho ya Mungu iko katika pua yangu;)
4Hakika midomo yangu haitanena yasiyo haki,
Wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.
5Hasha! Nisiwahesabie ninyi kuwa na haki;[#Ayu 13:15]
Hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu wangu.
6Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha;[#Ayu 2:3; Mdo 24:16]
Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai.
7Adui yangu na awe kama huyo mwovu,
Na mpinzani wangu awe kama asiye haki.
8Maana tumaini la mpotovu ni nini, ingawa ajipatia faida,[#Mt 16:26]
Hapo Mungu amwondoleapo roho yake?
9Je! Mungu atakisikia kilio chake,[#Mit 1:28; Isa 1:15; Mik 3:4; Zek 7:13; Yak 4:3]
Taabu zitakapomfikia?
10Je! Atajifurahisha katika Mwenyezi,[#Ayu 22:26]
Na kumlingana Mungu nyakati zote?
11Nitawafundisha ninyi mambo ya mkono wa Mungu;
Hayo yaliyo kwa Mwenyezi sitayaficha.
12Tazama, ninyi nyote mmeyaona wenyewe;
Mbona basi mmebatilika kabisa?
13Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu,
Na urithi wa hao waoneao, waupokeao kwa Mwenyezi.
14Watoto wake wakiongezeka ni kwa upanga;[#Kum 28:32,41; Est 9:10; 2 Fal 10:6-10]
Na wazao wake hawatashiba chakula.
15Hao watakaosalia kwake watakufa kwa maradhi mabaya,[#Zab 78:64]
Wala wajane wake waliofiwa na waume hawataomboleza.
16Ajapokusanya fedha kama mavumbi,
Na kujifanyia mavazi kama udongo kwa wingi;
17Yamkini kuyatengeza, lakini wenye haki watayavaa,[#Mit 28:8; Mhu 2:26]
Nao wasio na hatia watazigawanya hizo fedha.
18Yeye hujenga nyumba yake kama mdudu,[#Omb 2:6]
Na kama kibanda afanyacho mlinzi.
19Yeye hujilaza hali ni tajiri, lakini ndio mwisho;[#Hes 20:26]
Hufunua macho yake, naye hayuko.
20Vitisho vyampata kama maji mengi;
Dhoruba humwiba usiku.
21Upepo wa mashariki humchukua, naye huondoka;
Na kumkumba atoke mahali pake.
22Kwani Mungu atamtupia asimhurumie;
Angependa kuukimbia mkono wake.
23Watu watampigia makofi,
Na kumzomea atoke mahali pake.